Kilichomfanya Okwi kuzimia Dk 5 chagundulika.. Soma hapa


Straika wa Simba, Emmanuel Okwi akitolea nje ya uwanja kwa njia ya Machela baada ya kuumia na kuzimia kwa muda



BAO kali na la aina yake limefungwa jana Jumapili na straika wa Simba, Emmanuel Okwi dhidi ya Azam FC dakika ya 19 akiwa nje ya eneo la hatari sekunde chache baada ya kupokea pasi ndefu ya kuburuza ya beki Hassan Kessy.
Straika huyo ambaye awali alishaapa kuifunga Azam jana, alifunga bao la maana akiwazidi ujanja mabeki wa Azam pamoja na kipa wao Mwadini Ally.
Walidhani kwamba Okwi atapiga krosi kwa wenzake lakini badala yake, alisogeza kidogo mpira mbele kisha akamchungulia kipa Mwadini na kupiga mpira ulioenda moja kwa moja ukagonga kidogo mwamba wa juu na kutumbukia langoni.
Azam ilitumia dakika 57 kuwaziba midomo Simba baada ya kusawazisha kupitia kwa Kipre Tchetche. Azam ilionekana kutulia na kutawala sehemu kubwa ya mchezo ingawa wachezaji vijana wa Simba nao walionyesha juhudi na ufundi wa aina yake.
Nyuma ya tambo hizo za Simba, Yanga ilikuwa inaomba muda wote Simba iendelee na sare kama ilivyokuwa kwenye mechi za kwanza za msimu huu. Simba ilitulia na kucheza soka la uhakika na kuizidi Azam ambayo ilimtumia straika Didier Kavumbagu kuongoza mashambulizi,hata hivyo bao la Simba lilidumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili Simba, ilimtoa Elius Maguli na kumuingiza Simon Sserunkuma na Azam iliwatoa Frank Domayo na Didier Kavumbagu na nafasi zao zilichukuliwa na Khamis Mcha na John Bocco.
Mabadiliko hayo yaliisaidia Azam ambayo ndiyo klabu binafsi tajiri zaidi Afrika Mashariki, ilipata bao dakika ya 57 lililofungwa na Kipre Tchetche aliyepokea pasi safi ya Mcha ambaye ni tegemeo la Zanzibar Heroes.
Baada ya kuingia kwa bao hilo, timu zote zilicheza kwa kushambuliana kwa zamu lakini Simba ilionekana bado ina tatizo la washambuliaji kuchoka mapema kwani waliruhusu mashambulizi mengi na kulazimika kumtoa Said Ndemla na kumuingiza Shaaban Kisiga aliyeimarisha kiungo.
Dakika za mwisho baada ya kuingia Kisiga, Simba ilizinduka na kulishambulia lango la Azam ikipata kona mfululizo ambazo hata hivyo hazikuweza kuzaa bao, mbaya zaidi Okwi aliumia dakika ya 61 alipogongana na Aggrey Morris wa Azam akiwa katika harakati za kufunga na nafasi yake ilichukuliwa na Awadh Juma.
Okwi alitolewa uwanjani na kuwahishwa katika chumba cha huduma ya kwanza uwanjani hapo ambako alitibiwa na kuzinduka baada ya dakika tano hata hivyo baadaye alikimbizwa hospitali ya Muhimbili na mpaka tunakwenda mitamboni alikuwa akifanyiwa vipimo zaidi.
Kwa sare ya jana Jumapili, Azam imebaki kileleni ikiwa na pointi 21 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 20. Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Simba, Goran Kopunovic alisema; “Nimeridhika na sare hii kwani Azam ni mabingwa watetezi pia ni timu kubwa kwa hiyo sare si matokeo mabaya.”
Kwa upande wake, Kocha wa Azam, Joseph Omog alisema; “Wachezaji wangu hawakuwa makini na nafasi tulizopata sasa tunajipanga na mchezo ujao.”

No comments