NDIYO BASI TENA: Yanga itasota sana kuvunja rekodi hizi za Simba
SIMBA na Yanga ni watani wa jadi. Jambo linalofanyika Simba kwa namna moja ama nyingine litakuwa na tambo kwa Yanga.
Simba ikishinda mchezo lazima itatoa tambo zake kwa Yanga na vivyo hivyo kwa upande wa pili. Hayo ndiyo maisha waliyoyachagua.
Yanga ndiyo bingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara
ikiwa imetwaa taji hilo kwa mara 24 na kuzipiku timu nyingine zote
zinazoshiriki ligi hiyo. Simba inafuatia katika rekodi hiyo baada ya
kulitwaa taji hilo kwa mara 18.
Licha ya rekodi hiyo, Yanga bado inafunikwa na
Simba kwenye rekodi nyingine za maana. Simba imefanikiwa kuweka rekodi
kadhaa ambazo Yanga itasota kuzifikia. Makala hii inazungumzia baadhi ya
rekodi za Simba ambazo Yanga inasota kuzifikia na kuzivunja.
Kucheza fainali Caf
Simba ndiyo timu pekee ya Tanzania iliyofanikiwa
kucheza fainali za Kombe la Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika (Caf),
ilikuwa mwaka 1993 wakati huo likijulikana kama Kombe la Caf. Simba
ilicheza fainali hiyo na Stella Abidjan ya Ivory Coast na kutoka sare
katika mchezo wa awali kabla ya kukubali kipigo cha mabao 2- 0 katika
marudiano jijini Dar es Salaam.
Licha ya Simba kupoteza mchezo huo ambapo
wachezaji wake waliahidiwa zawadi za magari kama wangeshinda, inasalia
kuwa timu pekee kutoka Tanzania Bara iliyofanikiwa kucheza hatua hiyo ya
fainali hizo. Yanga imewahi kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Nusu fainali klabu Bingwa Afrika
Simba inajiweza, hivyo ndivyo unavyoweza kusema
kwa lugha rahisi baada ya timu hiyo kufanikiwa kucheza nusu fainali ya
Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974. Simba iliondolewa katika hatua hiyo ya
nusu fainali na Mehala El Kubra ya Misri na kuzima ndoto za kucheza
fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika.
Rekodi hiyo ya Simba bado haijavunjwa mpaka hii
leo. Yanga kwa upande wake, ilifanikiwa kucheza robo fainali ya michuano
hiyo kwa mara mbili mfululizo mwaka 1969 na 1970 lakini haikuwahi
kufika zaidi ya hapo.
Mbali na rekodi hiyo, Simba bado inajivunia rekodi
ya kuwa timu ya kwanza kutoka Bara kufanikiwa kuiondosha timu ya Misri
katika michuano ya Afrika. Simba ilifanya hivyo mwaka 2003 baada ya
kuifunga Zamalek ya Misri ambayo ilikuwa bingwa mtetezi.
Post a Comment