ACHANA na ubingwa wa Kombe la Mapinduzi ilioutwaa Jumanne
usiku kwa kuifunga Mtibwa Sugar penalti 4-3, Simba ya sasa ni ya
kuogopwa na ina kiburi.
Saa chache tu baada ya kutwaa taji hilo, kocha wa
timu hiyo, Goran Kopunovic, amewataka wachezaji wake kusahau kabisa
kuhusu walichofanya katika michuano hiyo na amewataka moto huo
wauhamishie katika Ligi Kuu Bara.
Kocha huyo Mserbia mwenye ufahamu mkubwa wa soka
la Afrika akiwa amewahi kuifundisha Polisi Rwanda, amewaambia wachezaji
wake kuwa timu watakazokutana nazo katika ligi lazima zionje makali ya
vipigo kutoka kwao ili kuthibitisha ubora wao.
Katika msimamo wa ligi, Simba inashika nafasi ya 12 kati ya timu 14 ikiwa na pointi tisa tu baada ya kucheza mechi nane.
Keshokutwa Jumamosi timu hiyo itacheza na Ndanda
FC ya Mtwara ambayo ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 10 baada ya kucheza
mechi kumi. Mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona
mjini Mtwara.
Mapema jana Jumatano Kopunovic aliwasili Dar es
Salaam akiwa na kikosi chake wakitokea Unguja na kombe lao walilotwaa na
walitumia saa chache kwa mapumziko na mchana wakaenda Mtwara kujiandaa
na mechi dhidi ya Ndanda.
“Nashukuru tumefanikiwa kutwaa Kombe la Mapinduzi,
si taji kubwa sana, lakini imekuwa ni fursa ya kukijenga kikosi chetu,
nafurahi kuona timu imekamilika kila idara, tutafanya vizuri kwenye
ligi,” alisema.
“Nataka hamasa tuliyotoka nayo huku kwenye
Mapinduzi itupe nguvu ya kufanya vizuri kwenye ligi, morali ya juu ya
wachezaji inanipa nguvu na matumaini ya kufanya vyema hasa katika mchezo
wetu wa wikiendi (dhidi ya Ndanda).
“Unajua nimeambiwa Simba ilikuwa haipati matokeo
mazuri huku kila timu ikijitahidi kutoka nayo sare, nafikiri sasa mambo
yamebadilika na wanapaswa kutuogopa kwani tuna morali ya ubingwa na
wachezaji wangu wametulia na kufuata maelekezo vizuri.”
Kocha huyo anayeamini katika soka la kasi na pasi
za kuachiana haraka haraka, aliliambia Mwanaspoti kuwa kwa jinsi kikosi
chake kilivyo sasa, haoni timu itakayowasumbua tofauti ilivyokuwa mwanzo
kabla hajafika.
Okwi apiga mkwara
Straika Emmanuel Okwi naye amesema haoni sababu ya
kikosi chao kuendelea kupata matokeo mabaya kwenye mechi za ligi kwani
sasa kipo vizuri na ari ya kupambana kwa wachezaji wote kwenye timu iko
juu.
Post a Comment