Hizi ni Sababu zinazompeleka Gareth Bale Man United



MANCHESTER United inatajwa kwenye mpango wa kumsajili winga ghali duniani na supastaa wa Real Madrid, Gareth Bale.
Staa huyo wa Wales anahusishwa na uwezekano wa kurejea Ligi Kuu England ikiwa ni kipindi kifupi kupita tangu alipong’oka Tottenham Hotspur na kutua Santiago Bernabeu kwa uhamisho wa Pauni 86 milioni katika kipindi cha majira ya joto mwaka 2013.
Wakati dirisha la usajili la mwezi huu likiendelea kuwa wazi, mchezaji huyo anaripotiwa kutaka kujiunga na Man United inayonolewa na Mdachi, Louis van Gaal. Timu hiyo ipo kwenye mipango ya kuboresha kikosi chake ili kurejea kwenye ubora.
Bale anaweza kufungua milango na kurejea kwenye Ligi Kuu England kujiunga na Man United kwa kuzingatia sababu hizi.
Mashabiki wa Real Madrid hawamkubali
Licha ya kuwa na mwenendo mzuri na kiwango kisichoshaka katika kutikisa nyavu huku mabao yake akiyafunga kwenye mechi muhimu zikiwamo za fainali, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Copa del Rey mwaka jana, Bale bado ameshindwa kuwa kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo.
Hali hiyo ilizidi kuwa mbaya zaidi Jumamosi iliyopita wakati mashabiki hao walipochukua uamuzi wa kumzomea Bale kisa hakumpa pasi Cristiano Ronaldo, aliyekuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga. Ilikuwa kwenye mechi yao dhidi ya Espanyol.
Umaarufu wa Ronaldo pale Bernabeu
Uhusiano wa Ronaldo na Bale ndani ya uwanja siku zote umekuwa mzuri na wenye kuheshimiana. Lakini, staa huyo wa Ureno Jumamosi iliyopita alifanya tukio ambalo limemsababishia Bale matatizo makubwa na sasa anaonekana hafai kwa mashabiki wa timu hiyo.
Kwa umaarufu wake, Ronaldo alionyeshwa kikerwa na ubinafsi wa Bale katika mechi ya La Liga dhidi ya Espanyol kitu ambacho kiliungwa mkono na mashabiki wa timu hiyo. Licha ya kufunga mabao muhimu, Bale anaendelea kufunikwa na kivuli cha Ronaldo na hata kama hakufanya ubinafsi makusudi, lakini jambo hilo litaendelea kumfanya Bale aonekane si kitu.
Uhamisho wa Angel di Maria
Kama ilivyofanywa na staa wa zamani wa Real Madrid, Angel Di Maria alipoamua kujiunga na Man United mwaka jana jambo hilo linaweza kumshawishi Bale akaamua kufuata nyayo zake.

No comments