Hawa ndio wachezaji wanaoongoza kwa ushirikina Viwanjani..




KUNA baadhi ya maeneo nchini hayana hospitali yoyote na kama zipo basi ni umbali mrefu kutoka yalipo makazi yao. Hayana vituo vya tiba wala wataalamu wa afya. Licha ya jitihada za serikali kuingiza huduma hizo katika maeneo hayo baadhi ya watu hao wamegoma.
Unajua kwa nini wamegoma? Yawezekana hujui, jibu ni rahisi, wanaamini zaidi ushirikina. Hawa watu hawaamini kuwa mtu anaugua tu kawaida.
Hivi ndivyo ilivyo kwa baadhi ya wachezaji wa soka nchini hasa wa Ligi Kuu Bara. Wapo baadhi ya mashabiki wa soka nchini hasa wa Simba na Yanga imani zao zimelala katika ushirikina na huhesabu kila tukio la uwanjani na imani hizo.
Matukio ya hivi karibuni uwanjani, baadhi ya wachezaji na mashabiki wa Yanga wameonekana kuamini katika ushirikina. Hawaamini kabisa kama timu yao inaweza kufungwa kihalali. Hawaamini kabisa kama washambuliaji wao Kpah Sherman, Andrey Coutinho, Amissi Tambwe na Simon Msuva wanakosa mabao kwa sababu ya umakini mdogo.
Tambwe akikosa mabao mawili mfululizo watu wanaweza kuamini amelogwa. Hali ndivyo ilivyo kwa wengine mpaka mashabiki wao.
Achana na ushirikina wa siri unaofanywa na klabu mbalimbali nchini, Yanga imekuwa ikijionyesha katika matukio ya wazi. Mwanaspoti inakuletea matukio matano ya wazi ya kishirikina yaliyoihusisha Yanga moja kwa moja.
Dilunga na hirizi ya Neto
Machi 30, mwaka jana Yanga ilijihusisha kwenye moja ya tukio la kushangaza la kishirikina. Yanga ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 ndani ya dakika 10 pekee za mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Hakuna mtu aliyeamini kama hilo linawezekana. Wakati mchezo huo unaendelea kiungo wa Yanga, Hassan Dilunga alimfuata mwamuzi wa mchezo huo na kumweleza kuwa mshambuliaji wa Mgambo, Mohamed Neto ana hirizi kwenye bukta yake. Hapa ndipo uchizi ulipoanzia.
Mwamuzi wa mchezo huo alitaka kumkagua Neto ndani ya bukta ili kuthibitisha kama kuna hirizi jambo ambalo straika huyo alilikataa kabisa.
Mtafaruku huo ulipelekea Neto kupewa kadi mbili za njano na kutolewa nje ya wakati huo timu yake ikiongoza kwa bao hilo moja.
Matokeo ya mwisho ya mchezo huo Mgambo ilishinda kwa mabao 2-1 lakini gumzo kubwa lilibaki kwa kitendo cha mchezaji wa Yanga kudai kuwa mwenzake amebeba hirizi. Aliwahi kuiona wapi kabla?
Taulo la Ivo
Huu unaweza kusema ni uvivu wa kufikiri ama kuchoka. Kwenye pambano la watani wa jadi Simba na Yanga msimu uliopita, aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu katika hali isiyotarajiwa aliparamia taulo la kufutia mikono la kipa wa Simba, Ivo Mapunda na kulitupa nje ya uwanja baada ya kukosa mabao ya wazi kwenye mchezo huo. Hisia za Kavumbagu ambaye sasa anacheza Azam FC, kama zilivyokuwa kwa wachezaji wengine wa Yanga na mashabiki wao walioshangilia kitendo hicho zilikuwa kwenye ushirikina.
Waliamini kuwa mabao wanayokosa yalitokana na taulo hilo la Mapunda. Hata hivyo licha ya kuliondoa taulo hilo bado Yanga ilishindwa kupata mabao na mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Msuva na pochi Morogoro
Hii ilikuwa imani ya ajabu kweli. Ni aibu kwa mchezaji wa kiwango cha Simon Msuva ambaye kila mtu anaamini kuwa muda wake kucheza soka la Bongo umekwisha na anatakiwa kutafuta timu kubwa za nje, yeye anaamini katika ushirikina tena wazi. Hii ilikuwa kwenye mechi ya ufunguzi wa ligi msimu huu dhidi ya Mtibwa Sugar mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Septemba 20 mwaka jana.
Yanga ilikuwa nyuma kwa bao moja huku washambuliaji wa timu hiyo wakiongozwa na Msuva wakiwa wanalisakama lango la Mtibwa kama nyuki ili kusawazisha bao hilo. Hali ilionekana kuwa ngumu kutokana na umakini wa safu ya ulinzi ya Mtibwa na kipa Said Mohamed kuokoa michomo ya hatari.
Msuva alishindwa kuliona hilo. Alipoiona pochi ya kike pembeni ya lango la Mtibwa aliamini ndiyo inayozuia mabao yao. Uzalendo ulimshinda winga huyo mwenye kasi nchini na kuamua kuiparamia pochi hiyo na kuirusha nje ya uwanja. Hata hivyo hilo halikusaidia kwani Yanga ilijikuta ikiongezwa bao la pili. Mtibwa ilishinda mchezo huo kwa mabao 2-0.
Chimbua chimbua Kaitaba
Kwa bahati mbaya ama nzuri Yanga imekuwa na matokeo mabaya katika mechi nyingi ambazo wanahusisha ushirikina. Walipokwenda mkoani Kagera kucheza na Kagera Sugar, Yanga walijikuta wakiingia tena kwenye mambo ya kishirikina.
Baadhi ya mashabiki na watu kadhaa wakubwa ndani ya klabu hiyo walionekana wakifukua fukua vitu visivyoeleweka kwenye Uwanja wa Kaitaba ambako mchezo huo ungefanyika kesho yake.
Waliamini kuwa Kagera wameficha madawa uwanjani hapo ili waifunge Yanga. Licha ya fukua fukua hiyo, Yanga ilijikuta ikifungwa bao 1-0 na Kagera.

No comments