Jinsi Simba ilivyojipanga kutwaa ubingwa leo.. Soma hapa

 
KAMA mikwara ya nje ya uwanja ni ubingwa, basi Simba ni bingwa wa Kombe la Mapinduzi hata kabla ya fainali ya leo Jumanne usiku dhidi ya Mtibwa kwenye Uwanja wa Amaan hapa Unguja, Zanzibar.
Simba ambayo ina uzoefu na mechi zaidi za fainali kuliko timu yoyote nchini, imebadilika ndani na nje ya uwanja baada ya kufuzu hatua hiyo.
Tangu wikiendi iliyopita, viongozi wote wa juu wa Simba pamoja na wajumbe wa kamati zake, wamehamia karibu na kambi ya timu yao mjini hapa na kumekuwa na vikao vya mara kwa mara na wachezaji pamoja na kocha katika kuhakikisha wanazima kiburi cha Mtibwa ambayo katika siku za hivi karibuni imekuwa ikiitesa Simba kwenye michezo ya ligi na ile ya kirafiki.
Simba wamepandwa na mzuka hasa baada ya Yanga na Azam kung’olewa kwenye michuano hiyo ambayo waliokuwa mabingwa mtetezi KCCA ya Uganda walitolewa hatua ya robo fainali.
Habari za ndani zinadai kwamba vigogo watatu wa klabu hiyo wamevuka mipaka kwa kumpa kocha mpya, Goran Kopunovic kikosi ambacho wanataka kianze jambo ambalo vibosile wengine wakiongozwa na Rais Evans Aveva wamelikemea vikali na kumtaka kocha kutotoa ruhusa kwa watu kuingilia kazi zake.
Mashabiki wa Simba wameanza kumwagika kwenye viunga vya Zanzibar tangu juzi Jumapili jioni na jana Jumatatu bendera za rangi nyekundu zilitawala maeneo mengi ya Unguja ingawa Mtibwa nao walikuwa wajanja kwa kufanya mazoezi na programu zao sirini sana.
Mchezo huo utakaoanza saa 2:15 usiku, utazikutanisha timu zenye historia tofauti katika michezo mbalimbali ya fainali ambayo wameshinda mara 15 wakipoteza mara 7.
Wekundu hao wamecheza fainali za Mapinduzi mara nne na kuchukua mara mbili wakizifunga Mtibwa mwaka 2008 na 2011 wakiwafunga Yanga 2-0 huku wakipoteza dhidi ya Azam kwa mabao 2-1 mwaka 2012 na mwaka jana Mnyama alichapwa na KCCA mabao 2-0.
Mbali na mashindano hayo makali ya Simba katika mechi za fainali pia yalionekana katika Kombe la Kagame ambalo walichukua mara 6 ambazo ni nyingi kuliko klabu yoyote ya Tanzania hata Afrika Mashariki yote.
Rekodi za Simba kwenye fainali pia zinaonyesha Simba ilichukua kombe katika mechi za Kombe la Nyerere miaka ya 1984,1995,2000. Mtibwa wameingia fainali ya mapinduzi mara mbili miaka ya 2007 alifungwa na Yanga na 2008 ambapo walifungwa na Mnyama.
Mwaka 2009 ilichukua Kombe la Tusker dhidi ya URA ya Uganda, pia Mtibwa ikalichukua tena kombe hilo mwaka 2010 kwa kuifunga Ocean View, pia wamewahi kuingia fainali ya Kombe la ABC Bank mara moja na kufungwa na Simba mabao 3-2.
Simba iliyoweka kambi katika eneo lao la Mbweni Unguja na ikijifua katika Uwanja wa Chuo cha Ualimu Chukwani, itaingia uwanjani ikiwa na kikosi tofauti na kile kilichokubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Mtibwa katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi.

No comments