Bila shaka haya yamefanyiwa kazi
UTAMADUNI wa Simba miaka yote ni kucheza soka la kushambulia. Wachezaji wa timu hiyo wameangalia staili ya uchezaji ya timu hiyo kwa sasa wakaamua kumwelezea kocha wao Mserbia Goran Kopunovic ukweli ambao huenda ukasaidia kulinda kibarua chake.
Beki wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein
‘Tshabalala’ ndiye aliyekuwa wa kwanza. Amemwambia kocha huyo kwamba
anafurahishwa na soka la kushambulia kwani linamwongezea uhuru wa
kucheza.
Tangu kuwasili kwa Goran, Simba imeonekana kucheza
soka la kushambulia zaidi huku ikiwatumia mabeki wake wa pembeni,
Tshabalala na Hassan Kessy zaidi kama nguzo hiyo ya mashambulizi kwa
kusaidiana na mawinga.
Tshabalala alisema aina hiyo ya soka inamwongezea
uhuru wa kucheza kwani muda mwingi anapenda kupanda kwenda kusaidia
mashambulizi ya timu yao. “Napenda kupanda kwenda kusaidia timu katika
mashambulizi, kwa staili ya kocha huyu( Goran Kopunovic) napata uhuru wa
kucheza kwa kufunguka zaidi, kocha anapenda tushambulie,” alisema
Tshabalala
Mbali ya hilo, beki huyo alisema fursa aliyopata
ya kuaminiwa na kupewa nafasi katika kikosi cha kwanza inamwongezea
nguvu za kupambana kwani anafahamu fika kuwa akiteleza nafasi yake
itapotea kikosini hapo.
“Najua nje ya uwanja kuna wachezaji wazuri,
wanatamani kucheza kama mimi hivyo muda wote ninaokuwa uwanjani nacheza
nikiwa na hilo akilini, najitahidi pia kukumbuka majukumu niliyopewa na
kocha,” alisema Tshabalala
Beki huyo anakuwa miongoni mwa nyota wachache
waliosajiliwa na Simba msimu huu na kuingia moja kwa moja kwenye kikosi
cha kwanza cha timu hiyo akiwapiku mabeki wenzake Issah Rashid ‘Baba
Ubaya’ na Abdi Banda. Tshabalala amecheza mechi zote za Liigi Kuu msimu
huu hadi sasa pamoja na zile za Kombe la Mapinduzi.
Mkude: Kombinesheni imeiva
Kiungo wa Simba, Jonas Mkude amesema kwa sasa
kombinesheni yake na kiungo Said Ndemla imeiva na wanacheza kwa uelewano
wa juu tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Tangu kuwasili kwa Kopunovic, amekuwa akiwapanga
Mkude na Ndemla kwa pamoja katika nafasi hiyo ya kiungo. Awali alipokuwa
kocha Patrick Phiri alikuwa akiwapanga Mkude na Shabaan Kisiga ama
Awadhi Juma.
“Kwa sasa tunacheza vizuri, aina yetu ya uchezaji
pia inafanana kiasi, nadhani tunapoendelea kucheza pamoja tutaendelea
kuzoeana zaidi,” alisema Mkude baada ya timu yao kuifunga Ndanda FC
mabao 2-0 juzi Jumamosi.
“Kuhusu mchezo ulikuwa asilimia 50 kwa 50,
hatukuwazidi sana lakini tuliweza kuzitumia nafasi tulizopata vizuri,
Ndanda ni wazuri pia na wanacheza vizuri.”
Post a Comment