Yanga hii ni noma!

 SIMBA ina tatizo la kipa kutokana na makipa wake wawili tegemeo; Hussein Sheriff na Ivo Mapunda, kutokuwa fiti kutokana na majeruhi. Hivyo Kocha Patrick Phiri akapendekeza anunuliwe kipa wa Yanga mzoefu wa Simba, Juma Kaseja.
Wakati Kaseja na meneja wake wakiwa katika harakati za kuanza kusitisha mkataba ili kijana atue Msimbazi, Yanga wakamjazia Kaseja noti kwenye akaunti yake bila ya yeye kujijua ambazo sasa zinamfunga asiondoke ingawa hata mazoezi amesusa na hajatokea tangu waanze kupasha na Marcio Maximo kujiandaa na mechi ya Mtani Jembe dhidi ya Simba itakayochezwa Desemba 13.
Picha liko hivi; Kaseja anaweza kukwama kuondoka Yanga baada ya kubainika kwamba klabu hiyo imemuingizia fedha zake za usajili alizokuwa akiidai haraka kabla hajawasilisha barua ya malalamiko kusitisha mkataba. Lakini imebainika kwamba kitakachomwokoa Kaseja ni barua yake aliyowaandikia viongozi wake akitaka warekebishe baadhi ya vipengele kwenye mkataba.
Kaseja alisajiliwa na Yanga kwa Sh40 milioni lakini alipewa nusu huku wakikubaliana kummalizia nusu iliyokuwa imebaki. Hata hivyo Yanga walichelewa kummalizia fedha hiyo ambapo ilionekana kukiuka makubaliano ya mkataba wao.
Katika uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti umebaini kuwa tayari aliingiziwa fedha zake kabla ya meneja wake Abdulfatah Saleh kuwasilisha barua ya kusudio la kuvunja mkataba wake kwa kushindwa kulipa fedha hizo ambazo zilitakiwa kulipwa Januari 15 mwaka huu.
Chanzo cha habari kutoka Yanga, kililiambia Mwanaspoti kuwa baada ya Kaseja kuanza kulalamika, viongozi wa Yanga waliamua kumwingizia fedha zake kwenye akaunti ambazo tayari Kaseja imedaiwa anajua kama ziliingia hivyo barua yake ya kutaka kuvunja mkataba inaweza isiwe na nguvu.
“Kaseja aliingiziwa fedha zake zote muda mrefu, yeye alitakiwa kutumia busara tu kwa kutuomba viongozi wake kwamba anaomba akacheze timu nyingine ili kulinda kiwango chake na pia uamuzi wa kumpanga anao kocha, sidhani kama angezuiwa, lakini Yanga wameamua kummalizia fedha yake na ataendelea kubaki mpaka amalize mkataba,” kilisema chanzo hicho.
“Unajua wachezaji wetu wanashindwa kuelewa mambo madogo tu, wanakimbilia kuyaweka hadharani badala ya kuwafuata viongozi kuwauliza juu ya madai yao, Kaseja ameandika barua wakati tayari wameingiza fedha ingawa hazikuingizwa kwa muda uliotakiwa.”
Mwanaspoti ilipomtafuta Meneja wa Kaseja katika simu yake ya mkononi hakuweza kupatikana ingawa rafiki wa karibu na Kaseja aliliambia Mwanaspoti kuwa kwa sasa wanamsubiri Mwanasheria wake ambaye amesafiri.
Kocha Maximo amekuwa akimtumia kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ katika mechi zake zote kutokana na kuwa na imani naye.
Kaseja amekuwa akiwekwa benchi na sasa Mbrazili huyo ameonekana kukasirishwa zaidi baada ya Kaseja kuingia mitini kwenye mazoezi.

No comments