Utata juu ya Beki mpya wa Simba
SIMBA imekamilisha rasmi usajili wa kiungo wake mshambuliaji, Simon Sserunkuma anayetokea Express ya Uganda baada ya kupata hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) , lakini beki wa kati, Juuko Musheed, atalazimika kusubiri.
Akizungumza na Mwanaspoti akiwa na ushahidi wa nyaraka ya ITC ya Sserunkuma, Katibu Mkuu wa Simba, Steven Ally, alithibitisha hilo. Wakati ITC ya Sserunkuma ikipatikana imefahamika kwamba Musheed bado atalazimika kusubiri kwa muda kwa vile uhamisho wake umeshikiliwa kwa muda na Fufa (shirikisho la Uganda) kutokana na utata uliojitokeza kati ya klabu yake ya zamani ya Victoria University na Simba.
Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema Musheed usajili wake utalazimika kusubiri kwa muda kufuatia beki huyo kuwa na shauri katika kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ya Fufa ambalo bado halijapatiwa majibu.
“Tumewasiliana na Fufa kujua nini kinachokwamisha uhamisho huo licha ya kuombwa ndani ya muda na majibu tuliyoyapata ni kwamba mchezaji husika kule kwao ana shauri lililopo katika kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ambalo bado halijasikilizwa kwa hiyo Fufa hawawezi kukamilisha uhamisho wake mpaka hilo litakapopatiwa majibu,”alisema Wambura.
Post a Comment