Sserunkuma anena juu ya Kaseja
STRAIKA wa Simba, Dan Sserunkuma amesema kwamba kiwango alichofikia kipa Juma Kaseja alitakiwa kwenda kucheza soka la kulipwa na sio kujiunga Yanga baada ya kumalizika mkataba wake na Simba kwa kile alichoeleza kwamba uamuzi wake unammaliza kisoka.
Sserunkuma aliliambia Mwanaspoti katika mahojiano
maalumu kuwa, Kaseja ni miongoni mwa wachezaji aliokuwa akiwasikia na
alibahatika kumwona katika michuano ya Kombe la Challenji lakini
ameshangazwa kuona sasa hivi hadaki japokuwa amesajiliwa na timu kubwa
ya Yanga.
Alisema kuwa kwa sasa Kaseja siyo mchezaji tena wa
kuzichezea timu hizi kongwe nchini Simba na Yanga na badala yake
atafute timu nyingine nje ya nchi kama ilivyokuwa kwa kipa mwenzake, Ivo
Mapnuda, ili kujijengea heshima.
“Kuna kipindi nilisikia kuna timu ya nje
inamhitaji, kwa nini hakwenda huko? Unajua kwasasa hawezi kuonekana wa
maana kwani timu anazozichezea ni zile zile Simba na Yanga, hawawezi
kuona ubora wake, ni vyema angekwenda huko alikokuwa anahitajika kuliko
kwenda Yanga.
“Kaseja baada ya kumaliza mkataba na Simba
angeamua kwenda nje naamini angejenga heshima kubwa kama ilivyo kwa Ivo,
alitoka hapa akaenda Gor Mahia alijenga kiwango na heshima ndio maana
Simba wakamchukuwa tena, Kaseja si wa kukaa benchi,” alisema Sserunkuma.
Katika usajili wa dirisha dogo uliofungwa Desemba
15, Kaseja ambaye mwaka jana FC Lupopo ya Kongo DR walikuwa
wanamuhitaji, alikuwa anatajwa kurudi Simba baada ya kuiandikia barua ya
kusudio la kuvunja mkataba wake na Yanga kwa maelezo kwamba wamekiuka
mkataba kwa kushindwa kummalizia fedha yake ya usajili Sh 20 milioni
kati ya Sh 40 milioni walizokubaliana.
Hata hivyo, Yanga tayari wamemwandikia barua
wakili wa Kaseja ambaye ni Kampuni ya Mbamba Advocate ya kutaka walipwe
Sh 340 milioni ikiwa ni fidia ya usumbufu wa gharama za kuvunja mkataba
pamoja na fedha ya usajili wake.
Post a Comment