Sserunkuma huyu ni moto
USAJILI wa dirisha dogo kwa timu za Ligi Kuu Bara na Ligi Daraja
la Kwanza ulifungwa Jumatatu ambapo baadhi ya timu zimeweza kusajili
ili kuimarisha vikosi vyao, lakini nyingine hazijasajili kwa kuamini
ubora wa vikosi vyao.
Kila timu inatakiwa kuwa na wachezaji 30, lakini
timu nyingi katika usajili wa msimu huu hazikuweza kujaza nafasi zote
ambapo sasa wamejaza nafasi hizo katika usajili wa dirisha dogo. Timu
hizo ni pamoja na Simba ambayo imesajili wachezaji watatu wa kigeni
ambao ni Dan Sserunkuma, Simon Sserunkuma na Juuko Murshid ambao wote ni
raia wa Uganda. Dan na Simon hawana undugu wowote bali majina tu ndio
yamefanana.
Usajili wa Dan Sserunkuma ndiyo ulionekana
kutikisa katika timu hiyo ya Simba, ni kwa kuamini kwamba ni straika
imara kutokana na rekodi yake ya Gor Mahia ambapo amekuwa Mfungaji Bora
mara mbili mfululizo katika Ligi Ku Kenya (KPL), msimu wa 2012/13 na
2013/14.
Sserunkuma alicheza kwa kiwango cha juu na
kuisadia Gor Mahia kwa kiasi kikubwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu
wa 2012/13 ambapo alifunga mabao 17 na kuwa Mfungaji Bora wa msimu huo
na msimu wa 2013/14 alifunga mabao 16. Kwa muda aliokaa Gor Mahia
amecheza mechi 73 na kufunga mabao 49 kwenye mashindano yote.
Sserunkuma alikuwa anahitajika na timu ya FC
Banants ya Armenia inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini humo lakini straika
huyo aligoma kwenda kwani aliona Gor Mahia bado ni timu inayomfaa kwa
wakati huo ingawa timu hiyo bado ilionyesha nia hata wakati Simba
ikimuwania.
Pia, mwaka 2013, Sserunkuma alipata tuzo ya
Mchezaji Bora iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo
Uganda (USPA) akiwapiku wachezaji wenzake; Tony Mawejje anayecheza
Norway na Siraje Muhindo anayeichezea timu ya Chuo Kikuu cha Sayansi na
Teknolojia cha Mbarara (MUST).
Katika mahojiano na Mwanaspoti, straika huyo
aliweza kuelezea mambo mbalimbali katika soka hasa nini atawafanyia wana
Msimbazi hao katika mechi zilizobaki za ligi.
Nani amemleta Simba
“Hapa kuna rafiki zangu kama Emmanuel Okwi na
Joseph Owino, viongozi wa Simba waliponihitaji niliwauliza kwanza hao
jinsi maisha ya hapa yalivyo, kwani sikuwahi kuishi hapa zaidi ya kuja
mara moja tulipocheza na Simba mechi ya kifariki.
“Hivyo nilivutiwa sana na jinsi walivyonieleza
Okwi na Owino, niliona nije kujaribu kama nitaweza soka la hapa japo
soka la Afrika Mashariki halina tofauti sana ingawa Kenya wapo makini
katika soka lao na ndio maana wanatoka sana,” anasema.
“Baada ya kujiridhisha kutoka kwa Okwi na Owino,
nilikuja hapa, tulizungumza na kukubaliana jinsi ya malipo na nililipwa,
nilifanyiwa vipimo na kusaini siku hiyo hiyo, baada ya kumalizana nao
nilirudi nyumbani kwa ajili ya kujipanga kuja kuichezea Simba rasmi.
“Niliridhika na fedha niliyopewa na ndio maana
nilikubali kusaini mkataba na sikuona kama kuna sababu ya kwenda nchi
nyingine ambako kuna timu zilikuwa zinanihitaji, nitakuwepo Simba mpaka
nitakapomaliza mkataba wao kama nilivyoondoka Gor Mahia baada ya
kumaliza mkataba,” anasema Sserunkuma.
Post a Comment