Huu ndio mpango wa Pluijm
SASA mtaitambua Yanga. Imetangaza sekretarieti mpya iliyosheheni
wasomi kwenye fani mbalimbali pamoja na kutambulisha benchi jipya la
ufundi litakalokuwa chini ya Mholanzi Hans Pluijm ambaye naye amechimba
mkwara wa maana.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kupitia Mkuu mpya
wa Idara ya Habari na Mawasiliano Jerry Muro ametangaza sekretarieti
mpya itakayoongozwa na Katibu Mkuu, Jonas Tibohora. Omar Kaya
amekabidhiwa idara ya Masoko, Sheria amepewa Frank Chacha huku fedha
ikiongozwa na Baraka Deusdedit.
Ikaushie hiyo safu mpya. Pluijm alitangazwa
kuchukua nafasi ya Mbrazil Marcio Maximo aliyesitishiwa mkataba wake na
klabu hiyo alisema baada ya kuona ubora wa wachezaji wake wa zamani na
wale wapya washambuliaji Amissi Tambwe raia wa Burundi, Mliberia Kpah
Sherman na mzawa Danny Mrwanda kazi ya kuunda kikosi hicho itaanza rasmi
leo Jumamosi.
Amesisitiza kwamba kurudi kwake Yanga anataka
kurudisha nguvu ya soka la kushambulia litakaloambatana na nidhamu ya
uwanjani na nje ya uwanja ambapo amewataka mashabiki wa timu kumpa siku
saba tu afanye mambo yake na wamiminike kwenye Uwanja wa Taifa kuangalia
mambo yake dhidi ya Azam FC watakaoumana nao Desemba 28.
“Nafurahi kuona kwamba kila mtu ndani ya Yanga
anafurahia ujio wangu, nawaomba mashabiki wa Yanga na wanachama wenzangu
watulie watuachie nafasi tuitengeneze timu mimi na msaidizi wangu
Charles (Mkwasa),” alisema Pluijm ambaye Mwanaspoti linafahamu kwamba
amesaini mktaba wa mwaka mmoja na nusu.
“Naijua Yanga, hii ni timu yangu, najua natakiwa
kuanzia wapi kurudisha nguvu yake iliyopungua hivi karibuni, nataka
kuwaona wachezaji wote kesho (leo) nasikia kuna wapya nataka kujua ubora
wao baada ya hapo nitaanza kurudisha nguvu ya timu,”alisisitiza kocha
huyo kwa kifupi huku akiwakumbushia mashabiki jinsi alivyoinoa Yanga
iliyoitoa ulimi nje Al Ahly ya Misri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Habari kutoka ndani ya uongozi zinasema kwamba
Pluijm ameona video za mechi za Yanga na kusema matokeo ya kutoridhisha
ya timu hiyo yametokana na mambo mengi ikiwemo wachezaji kukosa ari ya
kupambana.
Kwa mujibu wa kigogo mmoja wa Yanga, kocha huyo
aliomba kuona vipande vya video hizo za mechi za Yanga na kugundua vitu
kadhaa ambavyo viliigharimu timu. “Alipoona video hizo, ametuambia kuna
vitu havipo sawa katika timu kwanza hiyo ari ya kupambana kwa wachezaji
haipo kabisa kwani wachezaji wanakuwa kama hawana uchungu na timu na
wanacheza huku wakikosa umakini,” alisema.
Katika hilo kocha huyo amewahakikishia atarejesha
uwezo wa pumzi kwa wachezaji wote ili waweze kupambana kwa dakika zote
uwanjani lakini kwa kucheza soka la kuonana na siyo kutegemea mipira
mirefu pekee.
Bosi huyo amewaambia mabosi wake kwamba mabeki
lazima wakabe kwa akili na kucheza soka la kuonana na siyo kuharakisha
kupiga mipira mirefu kwani ni rahisi kwa adui kuinasa na kuweka chini
kisha kuwamaliza.
Post a Comment