Simba yamtisha Haruna Niyonzima
KIUNGO wa Yanga, Haruna Niyonzima, ameitazama Simba ya sasa na kusema wachezaji wake wengi wanacheza kwa kujiamini.
Niyonzima raia wa Rwanda, alisema tofauti na
walivyocheza mechi za nyuma katika Ligi Kuu Bara, sasa wachezaji wengi
wa Mnyama wanaonekana kubadilika na kucheza soka la kujiamini na wana
uwezo wa kupambana kwa dakika zote.
“Simba wanajiamini sana sasa hivi na hii ni
tofauti na walivyokuwa wakicheza mwanzo katika ligi, hawakuwa vile kama
walivyocheza,” alisema.
“Kama wakitulia na kucheza vile kila siku, basi
watakuwa na ushiriki mzuri katika ligi na kuweza kupata mafanikio. Hata
hivyo na sisi Yanga hatupo vibaya sana kwani tuna timu nzuri ya
ushindani ambayo inaweza kupambana na timu yoyote ile.”
Licha ya kuifunga Yanga mabao 2-0 wikiendi
iliyopita katika mechi ya Nani Mtani Jembe, Simba ilipata ushindi mara
moja tu katika mechi saba za ligi ilizocheza na kujikuta ipo nafasi ya
saba ikiwa na pointi tisa.
Simba itacheza mechi yake nyingine ya ligi Desemba
26 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Novemba
Mosi mwaka jana Simba ilipocheza na Kagera Sugar kwenye uwanja huo,
timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 na kutokea vurugu.
Post a Comment