Kaeni mbali na Simba hii
BAADA ya kuifunga Yanga mabao 2-0 katika mechi ya Nani Mtani Jembe, mshambuliaji wa Simba Mganda Emanuel Okwi, ametamba na kutamka kuwa sasa kazi imeanza Msimbazi wapinzani wakae mbali.
Katika mchezo huo, Okwi alicheza huku akipambana
kuhakikisha timu yake inashinda na kuonekana kuwa na hamu ya kuifunga
Yanga ambayo aliichezea msimu uliopita na kuamua kuachana nayo baada ya
kushindwa kummalizia fedha yake ya usajili.
Okwi aliliambia Mwanaspoti kuwa aliamini kwamba
Simba ingeshinda mechi hiyo kutokana na wapinzani wao kujiamini kwa
asilimia kubwa kuwa wangewafunga na kusisitiza kuwa timu yao ni nzuri na
itafanya vizuri katika mechi zijazo za Ligi Kuu.
“Naamini tutafanya vizuri kwenye ligi, huu ni
mwanzo tu, ubora wetu utaonekana kwenye ligi,” alisema Okwi ambaye
amebahatika kucheza mechi zote saba za ligi na kufunga mabao matatu.
Katika msimamo wa ligi, Simba inashika nafasi ya
saba ikiwa na pointi tisa na imeanza maandalizi ya Ligi Kuu ambapo mechi
yao ya raundi ya nane watacheza Desemba 26 dhidi ya Kagera Sugar,
mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Post a Comment