Sekunde 180 zilivyoiponza Yanga
WATU kimya na wala hakuna shabiki wa Yanga aliyekuwa na hamu ya kusimulia au hata kukumbuka matukio yaliyotokea uwanjani katika mchezo wao wa juzi Jumapili dhidi ya Simba ambao timu yao ilifungwa mabao 2-0.
Huo ulikuwa mchezo wa kirafiki wa Nani Mtani Jembe
ambao kabla ya kuanza mashabiki wa Yanga walikuwa na uhakika wa timu
yao kuibuka na ushindi huku Simba wakionekana kuwa tayari kwa lolote
lile.
Kama utani Simba ilicheza kwa kutulia zaidi
ikijipanga kwa mashambulizi ya hesabu huku Yanga wakiendelea na kawaida
yao ya kucheza na jukwaa, lakini mambo yaliwaharibikia na kujikuta
wakiruhusu mabao mawili kabla hata ya dakika 45 za kwanza kuisha.
Tofauti na Simba ambayo ilifanikiwa kurudisha
mabao matatu Oktoba 20, mwaka jana baada ya kuwa nyuma kwa mabao 3-0
hadi timu zinakwenda mapumziko katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara ambao
uliisha kwa sare ya mabao 3-3.
Mambo yalikwenda vizuri hadi wakati wachezaji
wanatoka katika vyumba vya kubadilishia nguo na kujiandaa kurudi
uwanjani kuanza kipindi cha pili. Hata hivyo kuna vitu vichache
vilivyotokea katika nukta chache za kutoka chumba hicho hadi mlango wa
kuingia uwanjani kwa muda wa dakika tatu hivi ambazo ni sekunde 180;
Mzozo chumbani
Hata kama Kocha wa Yanga Marcio Maximo alitoa
maelekezo kwa wachezaji wake, hali ilionekana ni ya kulaumiana miongoni
mwa wachezaji wa Yanga kwani hawakuwa na kauli moja na kwa dakika mbili
walikuwa wakitulizana na kuombana kuacha kulaumiania.
Muda huo ulifaa kwa kila mchezaji kutafakari na
kutulia kutazama watatumiaje maelekezo ya kocha kusawazisha makosa yao.
Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima alitumia muda mwingi kumtuliza nahodha
wake Nadir Haroub ‘Cannavaro’ asiwe na presha na mchezo huo.
Watoto wa kocha
Wachezaji wengi wa Yanga walionekana kulaumu
waziwazi kitendo cha Maximo kuwang’ang’ania wachezaji raia wa Brazil,
Emerson Roque na Andrey Coutinho kwani wenzao walidhani wachezaji hao
ambao wamebatizwa jina la ‘Watoto wa Kocha’ hawakuweza kuendana na kasi
ya mchezo huo.
Hapa wachezaji walionekana kumlaumu zaidi Maximo
kwa kuendelea kumuacha Emerson uwanjani. Akili zao hazikuweza kutulia na
nafsi zao zilishikilia kuwa kocha wao Maximo hakuwa akitendea haki
kikosi chake.
Post a Comment