Usajili wa Simba watikisa
Juku Musheed
SIMBA imesajili kikosi ambacho ni tofauti kabisa na kile cha mechi saba za Ligi Kuu Bara ilizocheza na tayari imetangaza kuwa ni muda wa maumivu kwa timu pinzani.
Dirisha dogo la usajili linakamilika rasmi leo
Desemba 15 saa sita usiku. Simba imewasajili wachezaji wawili wapya
kutoka Uganda na kuvunja mikataba ya wachezaji wawili wa Burundi.
Ni kama usajili huo umechagizwa na mechi ya juzi
Jumamosi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga ambapo Simba ilipata ushindi
wa mabao 2-0.
Kamati ya Usajili ya Simba, baada ya kikao cha
muda mfupi ilikubaliana na benchi la ufundi kuwasajili beki wa kati Juku
Musheed kutoka Victoria Univercity FC na Simon Sserunkuma wa Express.
Timu zote za Uganda.
Musheed anamudu kucheza beki ya kati na Sserunkuma
anamudu kucheza kiungo. Pia inaelezwa wakati wowote leo inaweza
kumalizana na beki David Owino kisha ikamkata Joseph Owino.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia
Hans Poppe ameliambia Mwanaspoti kuwa tayari wameshamsainisha Musheed
mkataba wa miaka mitatu huku wakiwa katika hatua za mwisho kumsainisha
Sserunkuma mkataba wa miaka miwili.
Hans Poppe alisema usajili wao unakamilisha idadi
ya wachezaji watatu ambao wamesajiliwa kwa sasa ambao ni Musheed,
Sserunkuma na Dann Sserunkuma lakini kiongozi mwingine wa Simba
aliongeza wamevunja mikataba ya Amissi Tambwe na Pierre Kwizera wote
raia wa Burundi na winga Uhuru Selemani.
Simba pia imesimamisha mkataba wa Raphael Kiongera
kwa muda wa miezi sita ili aimarishe afya yake kwani anasumbuliwa na
maumivu ya goti na ataendelea na mkataba wake wa miaka miwili ifikapo
Juni mwakani.
Kwa sasa Kiongera yupo katika matibabu India na
anarejea nchini Desemba 25, mwaka huu. “Tambwe na Kwizera tumeshavunja
mikataba yao rasmi leo hii (jana Jumapili) na sasa wanasubiri kulipwa
fidia zao za mishahara ya miezi sita kila mmoja, zoezi ambalo
litakamilika kesho (leo),” alisema kiongozi huyo.
Akizungumzia uamuzi huo, Tambwe aliliambia
Mwanaspoti: “Kweli nimekubaliana na Simba kuhusu kuvunja mkataba na sasa
tunasubiri kulipwa fedha zetu mimi na Kwizera ili tuondoke. Nimekubali
kwa shingo upande kwani unadhani tutaenda wapi?”
Akizungumzia uamuzi huo, Kocha Phiri alisema:
“Tambwe na Kwizera siyo wachezaji wabaya lakini kutokana na kuja kwa
changamoto mpya imebidi ufanyike uamuzi mwingine ambapo ilikuwa ni
lazima wawili wakatwe ili tuwasajili hao, naamini kikosi kitakuwa imara
zaidi kwenye mechi zijazo.”
Kuna uwezekano mkubwa wa Kwizera kupata timu
katika nchi za Rwanda, Malaysia, Dubai na Afrika Kusini ambako imeelezwa
kuna timu zimekuwa zikimhitaji.
Post a Comment