Mliberia amuumbua mtu
Mliberia wa Yanga, Kpah Sherman
NI kama amemuumbua lakini amemtumia kufikisha ujumbe kwa mashabiki na timu pinzani kwamba yeye ni straika mkali. Mliberia wa Yanga, Kpah Sherman jana amempiga Ally Mustapha ‘Barthez’ hat trick mazoezini.
Katika mazoezi hayo ya jana Jumatatu asubuhi
kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, Kocha wa Yanga, Marcio
Maximo alitumia muda mrefu kuwaelekeza mabeki wake jinsi ya kuokoa
mipira kutoka pembeni hasa ya juu.
Wakati wote wa mazoezi hayo, langoni alikuwa kipa
namba mbili Ally Mustapha ‘Barthez’ ambaye alionekana kuwa makini
akisaidiana na mabeki wa kati Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin
Yondani.
Zoezi hilo lilihusisha mipira ya krosi ambayo
Yanga ilionekana kutokuwa makini kuokoa katika mchezo wao dhidi ya Simba
wikiendi iliyopita ambao uliisha kwa Simba kushinda mabao 2-0.
Mazoezi hayo yalihamia kwa washambuliaji wa timu
hiyo kupewa mbinu za kufunga kwa kutumia mipira hiyo ya krosi ambao
walioonekana kuwekewa mkazo ni beki Cannavaro na straika Mliberia Kpah
Sherman.
Sherman, ambaye mashabiki wa Yanga wamemkubali kwa
roho moja kutokana na uwezo wake, alimfundisha soka Barthez na kumpa
mambo ambayo yamemtofautisha na mastraika wengine, alimfunga mabao
matatu yaliyoenda shule. Straika huyo amechukua nafasi ya Hamis Kiiza wa
Uganda aliyeachwa na Marcio Maximo.
Katika mechi ya kirafiki ya Nani Mtani Jembe,
Yanga ilifungwa bao la pili na Elius Maguli baada ya mabeki wake
kutokuwa makini kuokoa mpira wa kurushwa kutoka upande wa kulia, hivyo
Maximo ametaka kuhakikisha makosa hayo hayatokei tena. Yanga ililala
mabao 2-0 dhidi ya Simba.
SHERMAN ANENA
“Ninachotazama sasa nikuhakikisha najituma zaidi
ili Yanga ipate mafanikio, nimeona ipo nafasi ya pili katika msimamo na
idadi ya mechi inalingana na timu zote, nawahakikishia mashabiki wa
Yanga kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kutwaa ubingwa kwani tuna timu nzuri
ya ushindani,” alisema Sherman.
Hata hivyo Sherman aliyesajiliwa na Yanga kutoka
klabu ya Centikaya ya Cyprus alilazimika kutoka baada ya kuumia dakika
ya 62 na nafasi yake akaingia Mrisho Ngassa.
“Mchezo wa Simba umenifanya nihisi nina kazi ya
kufanya na naamini nitaweza kuipa matunda Yanga kwani najiamini naweza,
idadi ya mashabiki ilinishangaza kwa kweli,” alisema Sherman
Post a Comment