Yanga yatibua mipango ya Simba tena..!

Deus Kaseke
KWANZA Yanga ilitaka kumsainisha, Jonas Mkude, wa Simba lakini Mnyama akakaza mpaka dakika ya mwisho na saa chache kabla ya Yanga kupanda dau, Simba wakamaliza kazi na kijana akabaki Msimbazi.   
Wiki hii Simba ilimleta Dar es Salaam kiraka wa Mbeya City, Deusi Kaseke, kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo ya kumsajili kwenye dirisha dogo ambalo linafungwa Desemba 15.
Yanga ikaingilia kati na kufanya mazungumzo ya siri na mchezaji huyo, lakini akagoma kumaliza dili hilo baada ya Yanga kushindwa kufika dau lake la Sh40 milioni, Simba nao wakashindwa kumsainisha kwa vile walitaka kumpa Sh20 milioni kwa mikupuo miwili na dili hilo pia akalipiga chini.
Sasa unajua Yanga walichofanya? Wamemfuata Kaseke Mbeya kumweka sawa na huenda mambo yakamalizika wikiendi hii, Mwanaspoti linajua mchongo wote na mazungumzo yamefanyika kwa kina jana Ijumaa na yataendelea leo Jumamosi kwa kumhusisha mshauri wa karibu wa mchezaji huyo.
Ikaushie hiyo ya Mbeya. Jana Yanga ilianza pia mazungumzo na kiungo mchezeshaji wa Mgambo JKT, Sabri Makame ‘Momo’ na Mwanaspoti linaweza kuthibisha jinsi timu yake ilivyoshtukia ishu na inahaha kumdhibiti kijana asipokee mshiko wa matajiri wa Yanga.
Yanga ilimpigia simu juzi akiwa kwao Zanzibar na kumtaka aje Dar es Salaam kwa mazungumzo, lakini viongozi wa Mgambo wameshitukia janja hiyo na kumtaka mchezaji huyo aende Tanga haraka kujiunga na wenzake kambini.
 Yanga baada ya kugundua mkataba wake ni mrefu kidogo wakaona isiwe shida wakamwambia mchezaji atangulie Tanga watamfuata kambini haraka iwezekanavyo.
Makame alipotafutwa na Mwanaspoti alisema: “Siwezi kukataa ofa yoyote iwapo ni nzuri na inayoweza kunisaidia maishani. Mimi ni Askari wa kikosi cha jeshi la JKT Mgambo, lakini natafuta maisha.
“Yanga walinitafuta lakini siwezi kusema lolote kwasababu mimi ni mali ya JKT kwa sasa, lakini iwapo wamedhamiria ninaweza kung’oka na kuacha uaskari na kujiunga nao, pesa ndiyo kila kitu.
“Naamini kipaji nilichonacho, umri wangu mdogo unanipa fursa hiyo na nitaweza kufanikiwa kama walivyofanikiwa kina Mwinyi Kazimoto na Hassan Dilunga ambao walikuwa na timu za Jeshi.”
Katibu Mkuu wa Mgambo, Antony Mgaya alisema: “Hatuwezi kumzuia mchezaji kuondoka, kila mmoja ana nafasi ya kuondoka kwenda kutafuta maisha. Cha msingi iwapo mchezaji ni askari anajua utaratibu wa kijeshi na ule utaratibu wa kuvunja mkataba hivyo kama kuna timu inahitaji wachezaji wetu wanaruhusiwa kuja na kukaa na sisi mezani.”

No comments