Mkataba wa Okwi wayeyuka Simba, atishia kuondoka
MSHAMBULIAJI wa Simba, Mganda Emmanuel Okwi, amekaribia kumaliza mkataba wake wa miezi sita aliosaini wakati akijiunga na klabu hiyo mwanzoni mwa msimu huu na sasa tayari ameutaka uongozi kumpatia mkataba wa miezi mingine sita kabla ya mechi ya Mtani Jembe dhidi ya Yanga Desemba 13.
Okwi alijiunga na Simba akiwa mchezaji huru baada ya Yanga kuvunja mkataba naye baada ya kushindwa kukamilisha nusu ya malipo ya mkataba huo.
Mshambuliaji huyo alishindwa kusaini mkataba mrefu na Simba kutokana na Yanga kumfungulia kesi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambayo ilibidi imalizike kwanza.
Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Okwi hakusaini mkataba wa miaka miwili kama ilivyozushwa bali alisaini mkataba wa miezi sita na ndilo jambo linalowaumiza vichwa mabosi ya Simba kwa sasa kwani ametishia kwamba kabla ya mechi ya Yanga anataka kiwe kimeshaeleweka vinginevyo atatoweka.
Kocha wa Simba, Patrick Phiri alikiri kuwa Okwi bado alikuwa kwenye mazunguzo na uongozi juu ya kusaini mkataba mpya, lakini alishindwa kulizungumzia zaidi suala hilo kutokana na kuwa lipo nje ya mamlaka yake.
“Okwi ni mchezaji muhimu kwenye kikosi chetu kwa sasa, natumaini viongozi wamefika mahali pazuri ili kumsainisha mkataba mpya, kocha huwa sina mamlaka na kazi hiyo ya mikataba bali kwangu ni kutoa ripoti ya uwezo wa wachezaji na umuhimu wao ndani ya timu,” alisema Phiri.
Alipoulizwa juu ya suala hilo, Katibu wa Simba, Steven Ally alisema: “Siwezi kuzungumza chochote juu ya mikataba ya wachezaji, siwezi kukwambia juu ya mkataba wa Okwi ama mchezaji mwingine kwenye timu, hiyo ni siri yetu na wachezaji husika.”
Hata hivyo kauli ya Katibu hiyo imekuwa ni ya kushangaza kwani suala la mchezaji kusaini mkataba mpya huwa si kificho.
Mara nyingi kinachofichwa huwa ni makubaliano yaliyoko ndani ya mkataba husika kama maslahi na masharti ya kuvunja mkataba.
Post a Comment