Phiri aanzisha kasheshe jipya na Tambwe
Jambo hilo huenda likawa kasheshe zaidi kwa Tambwe kwani atalazimika kutumia nguvu kubwa zaidi kumridhisha Phiri ambaye anaonekana kutomkubali.
Kabla ya kuondoka, kocha huyo alifichua siri kuwa aliuomba uongozi wa klabu hiyo kumruhusu Tambwe aondoke, lakini straika huyo alimgomea na kutaka kuendelea na maisha kwenye klabu hiyo hadi kumalizika kwa mkataba wake mwishoni wa msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Mwanaspoti kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, kabla ya kuondoka kwenda Zambia, Phiri alisema kamwe hawezi kubadili mfumo ili uendane na aina ya uchezaji wa Tambwe, hivyo amemtaka straika huyo kujitahidi kubadilika ili afiti kwenye mfumo anaoutumia sasa.
Tambwe ameonekana kushindwa kufiti kwenye mfumo wa Phiri na kushindwa kung’ara tofauri na msimu uliopita alipoibuka mfungaji bora.
Kitu kinachompa Tambwe shida ni kitendo cha kocha huyo kuwataka wachezaji wote kurudi kukaba timu ikizidiwa na kupanda kushambulia kwa kasi kitu ambacho kimekuwa kigumu kwa Tambwe aliyezoea kufunga kwa kuvizia,
“Tambwe amesema haondoki, baada ya kugundua kuwa hana furaha na maisha ya Simba nilimshauri aondoke lakini amegoma, ni uamuzi sahihi alioufanya lakini inabidi ajiandae kufiti kwenye mfumo wangu,” Phiri alisema.
“Sina mpango wa kumbadilishia majukumu kwani anapaswa kucheza kama wachezaji wengine, anatakiwa kurudi kukaba pale tunapopoteza mpira na kupanda kushambulia pale timu inapokuwa na mpira.
“Tambwe anatakiwa achukue mfano kutoka kwa wachezaji mahiri kama Cristiano Ronaldo ambaye hushambulia lakini timu ikipoteza mpira utamkuta amerudi kusaidia kukaba, hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa.
“Sasa yupo Simba, lakini kesho hajui atakuwa timu gani, hafahamu timu hiyo itakuwa ikitumia mfumo gani hivyo ni vyema akajifunza kubadilika ili kuendana na mifumo tofauti tofauti.”
Mzambia huyo amekwenda kwao kwa mapumziko ya wiki moja na kusema kuwa amependekeza masuala kadhaa kwenye ripoti yake aliyokabidhi kwa uongozi ikiwemo suala la kambi ya timu ambayo ametaka lifanyike kwenye eneo tulivu kama ilivyokuwa visiwani Zanzibar kabla ya kuanza kwa msimu.
“Tuna mechi ngumu mbele, tutacheza na Yanga kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe, ni mechi ngumu kwani itatukutanisha watani wa jadi, ni lazima nishinde mechi hii kuwapa raha mashabiki wa Simba, nimependekeza kambi yake iwe eneo tulivu,” alisema Phiri
Post a Comment