Yanga yasajili mido mbili

Marcio Maximo
YANGA imepanga kusajili wachezaji watatu wapya mmoja ikifikiria atoke nje ya nchi.
Lakini Mwanaspoti limepenyezewa majina mawili ya wachezaji wa ndani ambao kocha Marcio Maximo anawataka.
Maximo amewaambia viongozi kwamba anataka beki wa kushoto na viungo wawili wenye uwezo mkubwa wa kukaba na kupandisha mashambulizi. Pia amewadokeza kwamba anataka mshambuliaji mwingine ambaye kuna uwezekano mkubwa akahatarisha ajira ya Hamis Kiiza ambaye hana namba kwenye kikosi cha kwanza.
Mmoja wa viongozi wa Yanga amelidokeza Mwanaspoti kuwa Maximo amewaonyesha wachezaji wawili viungo ambao wanacheza Mtibwa na JKT Ruvu.Ambapo kutoka Mtibwa amewaambia anamtaka Ally Shomary na JKT Jabir Aziz.
Habari zinasema kwamba Maximo alimkubali Jabir tangu alipokutana na Yanga kwenye mechi ya Oktoba 5 katika uwanja wa Taifa na Yanga kushinda mabao 2-1 na vilevile amevutiwa na nidhamu ya uchezaji ya Shomary.
Habari zinasema kwamba kocha huyo amewaambia viongozi kwamba wakishindwa kuwanasa wachezaji hao wapendekeze ambao uchezaji wao unafanana nao hao kwani anataka watu wa kushambulia na wanaoweza kukaa na mpira kiumakini.
Dirisha dogo la usajili wa Ligi Kuu Bara linafunguliwa leo Jumamosi na litafungwa Desemba 15 ambapo timu mbalimbali zitapata wasaa wa kurekebisha vikosi vyao tayari kuendelea na mzunguko wa kwanza Desemba 26. Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara umepangwa kumalizika Januari 31 mwakani huku msimu ukimalizika Mei 9.

No comments