Azam FC yamtolea macho Chanongo


 AZAM FC imeweka mezani majina ya winga, Haroun Chanongo, Amri Kiemba, Said Ndemla wa Simba, straika Ame Ally wa Mtibwa Sugar,  kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima wa Yanga lakini inafanya mpango wa kumnasa mshambuliaji wa kigeni atakayetua muda wowote wiki ijayo.

Haya ni maagizo kutoka kwa kocha wao mkuu, Mcameroon Joseph Omog ambaye aliwasilisha ripoti yake kwa uongozi kwa kusema, anataka asajiliwe wachezaji wa ukweli kwa nafasi za kiungo mshambuliaji, winga pamoja na straika.
 Azam inaamini Chanongo au Ndemla ni chaguo sahihi, lakini hofu yao ni Simba ambayo tayari imewapa woga baada ya kudai dau la Sh15 milioni baada ya kumhitaji Kiemba.
Mwenyekiti wa Azam, Said Mohamed alisema: “Kocha anataka aongezewe wachezaji kwa nafasi za kiungo mshambuliaji, winga na straika. Amependekeza aina ya wachezaji anaowahitaji nasi kama uongozi tunaangalia yupi atakayetufaa.
“Tunafanya mchakato na kujadiliana hapa na pale ili kupata chaguo sahihi la atakayetusaidia. Mchezaji ambaye tulianza naye ni Kiemba ambaye kweli tuliwaandikia barua Simba  nao wakatujibu, sasa tunaendelea na taratibu nyingine.”
Lakini uchunguzi wa Mwanaspoti umepata majina ya wachezaji hao, Chanongo, Kiemba, Ame, Ndemla na Niyonzima. Pia baada ya Mmali Ismaili kufungashiwa virago vyake na nafasi yake akasajiliwa Muivory Coast Pascal Wawa, Azam inataka kumwondoa mgeni mwingine na kumsajili mpya.

No comments