Wenger adai Sanchez atatisha zaidi
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger
MTAMKOMA tu. Lazima mnune. Hakuna jinsi. Licha ya ushindi wa
mabao 2-1 dhidi ya Crystal Palace juzi Jumamosi jioni katika Uwanja wa
Emirates, kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, amedai kwamba staa wake mpya,
Alexis Sanchez, atatisha zaidi msimu huu.
Sanchez aling’ara katika pambano hilo, lakini
Arsenal walijikuta wakisubiri bao la dakika za majarehi la Aarona Ramsey
kuweza kuondoka na pointi tatu muhimu huku mahasimu wao wa zamani,
Manchester United wakilala mabao 2-1 nyumbani na Swansea City.
Sanchez alisaidia kupatikana bao la kwanza la
Arsenal lililofungwa na Laurent Koscielny na Wenger ambaye amemnunua
staa huyo wa Chile kwa dau la Pauni 30 milioni, ameonya kwamba mashabiki
wa Arsenal watalazimika kumvumilia nyota huyo mpaka atakapofikia
kiwango chake.
Wenger amesema Sanchez, 25, bado hajawa fiti na pia analazimika kuzoea maisha ya Emirates kabla ya kuwa katika hali ya kawaida.
“Nafurahishwa sana na tabia yake kwa sababu
anapigana kwa dakika zote 90 za mchezo ingawa bado hajawa vizuri
kimwili,” alisema Wenger mara baada ya pambano hilo.
“Kimbinu inabidi aimarike katika maelewano na
wachezaji wenzake. Lakini alionekana yupo safi muda wote mpaka mwishoni
mwa mechi. Nina furaha na kiwango chake na tabia yake pia.”
Kocha huyo Mfaransa pia alionekana kukoshwa na
kiwango kilichoonyeshwa na beki kinda, Calum Chambers ambaye mara nyingi
alikuwa mhimili mkubwa katika safu ya ulinzi ya Arsenal kwenye mchezo
huo uliofanyika wiki chache tu baada ya kuhamia kutoka Southampton.
“Lazima niwe mkweli, nilimnunua akiwa beki wa
kulia. Lakini kwa mtazamo wangu anaweza kucheza akiwa beki wa kati.
Nilijaribu katika mechi za mwanzo wa msimu na kila mechi amekuwa imara,”
aliongeza Wenger.
Kuhusu mechi, Wenger alidai kwamba mfumo wa
uchezaji wa Crystal Palace uliufanya mchezo kuwa magumu kwa vijana wake,
lakini akafurahishwa na matokeo.
“Walifanya mambo yawe magumu. Walijilinda vema na
wakatumia vema nafasi walizopata. Baada ya hapo wakabana katika nafasi
ya ulinzi. Walikuwa na nguvu zaidi na ilibidi lazima tuendelee kusonga
mbele tu.”
Post a Comment