Wacolombia wamfanyia sala maalumu Falcao

 

RIO DE JANEIRO, BRAZIL
MWAKA 2002 Waingereza walifanya sala kumwombea staa wao, David Beckham apone haraka mfupa wa mguu uliokuwa umevunjika ili aweze  kucheza fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Japan na Korea Kusini, lakini mwaka huu hilo limewakuta Wacolombia.
Kwa sasa wanapiga sala maalumu kumwombea straika, Radamel Falcao mwenye matatizo ya goti apone ili awemo kikosini kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa Brazil kuanzia Juni 12.
Wananchi wa Colombia kwa sasa hawana raha kabisa na wanasubiri taarifa za staa wao huyo kufahamu kama atakuwa fiti kucheza fainali hizo au la.
Falcao aliumia goti wakati akiitumikia klabu yake ya AS Monaco kwenye Kombe la Ufaransa Januari mwaka huu.
Colombia sasa imebakiza saa 24 kufikia uamuzi wa mwisho wa ama kumjumuisha staa huyo kwenye kikosi chake au iachane naye na hilo litaamuliwa kesho Jumapili na kocha Jose Pekerman atakapokitaja kikosi chake cha mwisho cha wachezaji 23 kitakachokwenda Brazil.
Falcao, ambaye alifunga mabao tisa katika mechi 13 za Colombia na kumaliza ya pili nyuma ya Argentina kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia kwa upande wa Amerika Kusini, alisema: “Hiki kinachofanywa na Colombia kinanipa hamasa. Kinaonyesha ni jinsi gani nilivyo muhimu kwa nchi yangu. Sisemi kinanipa presha, la kinanipa moyo zaidi wa kupambana. Nitafanya kila kitu si kwa ajili yangu, bali ni kwa ajili ya wananchi wote wa Colombia.
“Kadiri michuano hiyo inavyokaribia, naona umuhimu wake na sitaki kuwa mtazamaji tu. Nitafanya kila ninaloweza kuhakikisha nakuwa fiti. Lakini, majeraha yananirudisha nyuma na inanipasa kuwa mvumilivu tu. Inshallah Mungu mkubwa.”
Falcao ni miongoni mwa mastraika makini barani Ulaya na makali yake yaliifanya Monaco kulipa Pauni 51 milioni kuipata saini yake mwaka jana ilipomsajili kutoka Atletico Madrid.
Kabla hajatua Monaco, Falcao alikuwa akiwindwa pia na klabu za England ikiwamo Chelsea. Lakini, jambo kubwa kwa sasa kwa Wacolombia ni sala zao kuhakikisha nyota wao huyo anavaa jezi ya nchi hiyo Brazil na kufanya kweli kwenye mikikimikiki hiyo ya Kombe la Dunia. Daktari aliyemfanyia upasuaji straika huyo, Jose Carlos Noronha amewatoa hofu wananchi wa Colombia baada ya kuwaeleza kwamba mchezaji wao ana nafasi kubwa ya kucheza fainali hizo akifuta hofu kwamba atalazimika kukaa nje ya uwanja hadi msimu ujao.
Staa huyo ametajwa kwenye kikosi cha awali cha kocha Pekerman na amekuwa akifanya mazoezi mepesi na wenzake, lakini bado hakuna uhakika kama atakuwa fiti kwa kiwango kinachohitajika kuingia kwenye wachezaji 23 watakaoiwakilisha nchi hiyo kwenye fainali hizo.
 

No comments