Simba FC yaandaa mastraika watatu wa Mtani Jembe


PATRICK PHIRI.
SIMBA ina mechi mbili tu za maana za kumaliza mwaka.Ile ya Mtani Jembe dhidi ya Yanga Desemba 13 na ya ligi dhidi ya Kagera Sugar Desemba 26, kuna kitu kimoja ambacho Kocha Patrick Phiri amepanga kufanya.
Katika mechi ya Mtani Jembe ataisukumia Yanga moto wa aina yake kwa kuchezesha mastraika watatu kwa mpigo ili kuhakikisha wanashinda na lolote litakalotokea na lije kwani atafanya mabadiliko kama itabidi kwenye dirisha dogo linaloanza wikiendi ijayo.
Mastraika hao ni Elius Maguli, Amissi Tambwe na Emmanuel Okwi, walicheza kwa pamoja katika mechi ya ligi dhidi ya Ruvu Shooting juzi Jumapili na kuipa Simba ushindi wa kwanza tangu ianze msimu wa Ligi Kuu Bara ikiwa inacheza mechi ya saba. Simba ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Okwi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Phiri alisema atakomaa na wachezaji hao ili kurudisha  hadhi ya Simba halafu kama kuna mabadiliko ya kufanya itajulikana baadaye.
“Nimependa namna ambavyo Okwi, Tambwe na Maguli walivyocheza, walishirikiana vizuri na kutengeneza kombinesheni nzuri ambayo ilitupa ushindi.
Kutokana na namna walivyoelewana na kufanya vizuri, nafikiria kuwaanzisha wote kwa pamoja kikosi cha kwanza kwenye mechi ijayo(dhidi ya Yanga),” alisema Phiri ambaye alimwingiza Maguli kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Said Ndemla, ambaye mkataba wake na Simba unaelekea ukingoni.
Naye, Owino amesema: “Matokeo ya ushindi  ni kama tumetoa nuksi na kinachofuata sasa ni ushindi tu.”

No comments