Simba SC: Tumembakiza Mkude, tunamng’oa Twite

SIMBA mpaka jana Jumatatu jioni ilikuwa inakamilisha kumsainisha mkataba wa miaka mitatu kiungo wao, Jonas Mkude lakini Mnyama anaweza kuishangaza Yanga kwa kuishtukiza kwa kumng’oa Jangwani kiraka Mbuyu Twite ambaye amegoma kusaini mkataba mpya.
Mpaka jana mchana Simba ilikuwa imeshakubaliana na Mkude mambo mengi isipokuwa kulikuwa na utata kidogo kwenye masilahi.Mkude anahitajika Jangwani na tayari alishawaambia wampe Sh80milioni asaini.Lakini vigogo wa Simba walikuwa wametegesha kwamba kama wangeshindwa kumbakisha Mkude wangemng’oa Twite,lakini baada ya kufanikiwa kumdhibiti Mkude sasa wanamtaka na Mbuyu.
Habari za ndani kutoka ndani ya Yanga zinasema kwamba Mbuyu ambaye ni raia wa Rwanda mwenye asili ya DR Congo amebembelezwa na Yanga wiki kadhaa na bado ameshikilia msimamo kwamba haongezi mkataba mpaka masharti yake yatimizwe ishu ambayo Simba wameinasa na wameanza kuifanyia kazi kwa nguvu.
Habari zinasema kwamba Mbuyu ambaye amebakiza mkataba wa miezi sita unaomruhusu kuzungumza na klabu yoyote ile duniani, amesusa kwa madai kwamba Yanga walitaka kumsainisha kwa mali kauli huku wakiwa bado na deni lake kwenye usajili uliopita. Rafiki yake wa karibu aliidokezea Mwanaspoti kwamba anachotaka Mbuyu kwa sasa ni kulipa deni na kupewa fedha taslimu za mkataba mpya ambapo hata dau anataka lipande na mshahara uongezwe kidogo. Ingawa Yanga walikuwa wagumu jana kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo mmoja wa vigogo mwenye ushawishi mkubwa kwenye usajili wa Simba alisisitiza kwamba wanambakisha Mkude na wanamng’oa na Twite Yanga kwavile ana umuhimu mkubwa ndio maana walimtaka hata kabla hajatua Jangwani.
Yanga nao walikuwa na kikao jana mchana kujadili ishu ya Mkude baada ya kusikia kwa mambo hayajakaa sawa Simba. 
Lakini Mwanaspoti ilipomtaka Mbuyu kufafanua sakata lake aligoma kuzungumza hata neno moja kuhusiana na kugoma kusaini lakini akasema kama Simba ikimpa maneno matamu atafanya uamuzi mgumu.
“Waweke pesa mezani tuzungumze, tukikubaliana hakuna shida, kazi yangu ni mpira naweza kuchezea timu yoyote, kikubwa maslahi,”alisema Mbuyu na kukiri kwamba aliwahi kuzungumza na Azam kabla ya kusaini mkataba wa sasa unaomalizika Yanga.
Mwanaspoti ilimtafuta mke wa Mbuyu anayeishi naye Magomeni jijini Dar es Salaam, Bijuu Mbelenge alisema; “Kazi ya mpira ni sawa na mfanyabiashara,  penye maslahi makubwa ndio atakwenda. Lakini  soka iko tofauti na biashara nyingine kwa sababu ina muda.
Mchezaji anaweza akacheza kwa miaka 15 tu baada ya hapo anakwisha, kama haujajipanga utashindwa kufanya mambo mengine ya maendeleo.”
“Kama kweli hao Simba wanamwitaji Mbuyu, wafanye haraka tuzungumze,”alifafanua Bijuu ambaye ni Mkongomani. Mbuyu alisajiliwa na Yanga akitokea APR ya Rwanda lakini alikuwa chini ya FC Lupopo, klabu ambayo ilimlea na kumkuza kisoka.
Usajili wake kwenda Yanga ulikuwa na utata  kwani Simba chini ya uongozi wa Mwenyekiti, Ismail Rage ndio walikuwa wa kwanza kumsajili kutoka APR ya Rwanda lakini walidondokea pua baada ya sintofahamu ya makubaliano ya kimkataba.

No comments