MAFISADI WA IPTL KUANIKWA NOV 26

HATIMA ya vigogo wanaotuhumiwa kuchota fedha zaidi ya sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), itajulikana Novemba 26 mwaka huu,
wakati ripoti ya uchunguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), itakapowasilishwa bungeni na kujadiliwa.
Hatua hiyo ni baada ya Bunge kutuliza munkari wa wabunge kwa kuthibitisha kwamba hakuna barua yoyote iliyowasilishwa na Jaji Mkuu ili kuzima mjadala wa ripoti hiyo kama ambavyo imekuwa ikidaiwa.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Hassan Zungu, wakati akitoa mwongozo wake kuhusu madai kwamba Mahakama imeandika barua kwenda ofisi ya Spika kuzuia mjadala wa kashfa ya IPTL.
Mwongozo wa Zungu, ulitokana na kauli ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Moses Machali, kuhusu azimio la Bunge kuridhia itifaki ya uzuiaji wa vitendo haramu dhidi ya Miundombinu ya kudumu iliyojengwa chini ya bahari katika mwambao wa Bara wa mwaka 1998.
Katika hotuba yake, Machali alihoji kuna nini na akina nani wanaotakiwa kulindwa na mhimili wa Mahakama katika sakata la Escrow kiasi cha mahakama kuingilia uhuru wa Bunge.
Machali, alikumbushia kuwa wakati wa Bunge Maalum la Katiba, kulikuwa na kesi mahakamani, lakini bado Bunge hilo liliendelea na kuhoji iweje leo Mahakama ilizuie Bunge kujadili kashfa ya Escrow kwa kisingizio cha kuwapo kesi mahakamani.
Wakati akiendelea kuzungumzia kashfa ya Escrow na msimamo wa kambi rasmi ya upinzani, Zungu alisimama na kuamua kutoa taarifa ya kiti cha Spika.
“Nimesimama kutoa taarifa na naomba wabunge wengine mnaotaka kuchangia na kujielekeza katika jambo hili ni kwamba, Bunge halijapokea taarifa wala barua yoyote kutoka mahakamani kuzuia mjadala wa Escrow, jambo la pili mjadala wa ripoti ya CAG kuhusu uchunguzi wa kashfa hiyo itakuja bungeni kama ilivyopangwa,” alisema Zungu.
Hata hivyo, kauli hiyo ya kiti cha Spika imeibua hoja kutoka kwa baadhi ya wabunge kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Naibu Spika Job Ndugai, walipaswa kutoa kauli hiyo juzi, hivyo kusingekuwa na mjadala mkali uliosababisha Pinda kuzomewa.
Chanzo cha mjadala wa juzi ni majibu ya Waziri Mkuu Pinda aliyoyatoa wakati wa kipindi cha maswali ya papo hapo bungeni.
Pinda alilitibua Bunge kwa kuliambia kuwa kwa ufahamu wake kama mwanasheria, Bunge haliwezi kujadili ripoti ya CAG, kwa madai kuwa kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa mahakama.
Huku akiibua miguno na minong’ono kutoka kwa wabunge wengi wakiwemo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pinda alisema anachojua ni kwamba IPTL ina kesi zaidi ya kumi na wadau wake mahakamani ambao hazijaamuliwa.
Majibu ya Pinda yalitokana na swali la Moses Machali (NCCR Mageuzi), aliyehoji kuwa kuna taarifa kwamba Mahakama Kuu imeiandikia barua Bunge kuzuia ripoti ya CAG kuhusu kashfa ya Escrow, isijadiliwe bungeni na kumtaka Pinda atoe kauli ya Serikali.
Akifafanua zaidi jibu la swali hilo, Waziri Pinda alisema kwa maoni yake haoni kama ni sahihi kwa wabunge kujadili suala hilo nje ya Mahakama, kwani kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa Mahakama.
CCM wavutana
Katika hatua ya kutaka kukinusuru Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye kashfa hiyo, gazeti hili limedokezwa kwamba kumekuwepo na mvutano mkali ndani ya chama wa kuwalazimisha mawaziri na watendaji wengine wanotuhumiwa kuachia ngazi mapema.
Hata hivyo, mnyukano huo unaelezwa kutawaliwa na makundi ya urais wa 2015, ambapo wapambe wa watuhumiwa wanadaiwa kuwapa jeuri walengwa kwamba liwalo na liwe kwa vile hakuna aliye msafi.
“Kinachoendelea Dodoma sasa ni kutunishiana misuli, wale wanaolazimishwa kuachia ngazi wapambe wao hawakubaliani na hoja hiyo, wanataka ngoma (ripoti) ije ukumbini ili pambe zote ziumbuane kuhusu kashfa husika.
“Unajua ni kweli wako vigogo wataangushwa kwa kashfa ya kutafuna mabilioni hayo ya Escrow lakini ndani yake wako waliokuwa wanazunguka upande wa pili kuomba rushwa ili kuhakikisha wanazima sakata hilo na baada ya kukosa fedha hizo, wamekuwa vinara wa kutaka ripoti iletwe haraka watuhumiwa washughulikiwe,” kilisema chanzo chetu ndani ya CCM.

No comments