Yanga wamwiba kiungo mpya Simba hotelini Dar
KAMA sinema vile! Simba wamempandisha ndege na kumleta Dar es Salaam kiraka wa Mbeya City, Deus Kaseke na kumhifadhi kwenye hoteli moja maeneo ya Ubungo, Dar es Salaam, lakini Yanga walikuwa kimya wanafuatilia mchongo wote unavyokwenda.
Kuanzia Simba ilipomweka, dau wanalotaka kumpa na mshahara wanaopanga kumlipa kisha wakatafuta upenyo wakamvaa mchezaji huyo hotelini bila Simba kujua.
Yanga walitua kwenye hoteli hiyo na kumshawishi kisha kufanikiwa kumwondoa hapo na kumpeleka eneo jingine kabisa kufanya naye mazungumzo kwa lengo la kuipiga bao Simba, lakini wakakwama kwenye mambo kadhaa.
Yanga walimuahidi dau mchezaji huyo na kutaka kumuondoa kabisa kwenye hoteli ambayo alikuwa amepangishiwa na Simba wakamlaze sehemu nyingine wakati wanamalizana nae lakini Kaseke akakomaa akitaka kumalizana na Simba kistaarabu lakini vilevile akiisisitiza Yanga iweke fungu la maana mezani.
Ilikuwa hivi; Ndani ya saa 48 viongozi wa Simba na Yanga walijaribu kuzidiana akili kuhakikisha wanampata Kaseke ambaye bado ana mkataba wa miezi sita na timu yake inayosuasua kwenye Ligi Kuu Bara.
Vigogo wa juu wa Simba walizungumza na mchezaji huyo na kumuahidi kwamba watampa Sh20 milioni asaini mkataba wa miaka miwili, lakini walimwambia kwamba watampa nusu kwanza ili Desemba Mosi asaini halafu mapema mwakani amaliziwe kilichobaki naye akagoma kwa madai kuwa dau hilo ni dogo na anataka alipwe chake chote. Mchezaji huyo aliwakomalia Simba akitaka waongeze fedha kufikia Sh40 milioni ndipo asaini lakini vigogo hao nao wakamkomalia.
Baadaye Yanga wakamtafuta na kumpata kisha wakamfungia chumbani katika hoteli nyingine kwa mazungumzo ambapo wenyewe walifika dau la Sh22 milioni kwa vile tayari walishasikia kwamba Simba wanampa Sh20 milioni.
Habari za uhakika zinadai kwamba Simba walimpa mkataba akausome kisha awajibu lakini baadaye Yanga wakamtumia mtoto wa kigogo maarufu nchini ambaye ni mnazi wa Yanga kumlainisha Kaseke ikashindikana.
Yanga walimuahidi mchezaji huyo kiasi hicho cha fedha lakini mkononi aliyekuwa akimshawishi alikuwa na milioni moja tu, mchezaji huyo alivyoonyesha kwamba hana dalili ya kulainika akapigiwa simu kiongozi mmoja wa Mbeya City amshawishi lakini bosi huyo akadai kwamba hayo ni mambo binafsi hawezi kuingilia.
Habari ambazo Mwanaspoti ilizipata jana Alhamisi jioni kutoka Mbeya City ni kwamba wamemuongezea mshahara hadi Sh900,000 ili asiondoke na sasa anakuwa ndiye mchezaji anayelipwa ghali zaidi kwenye kikosi hicho kuanzia mwezi huu.
Licha ya kugoma kutoa ushirikiano katika sakata lake, Mwanaspoti linaweza kuthibitisha kwamba mchezaji huyo yupo Dar es Salaam na ataondoka kurudi Mbeya leo Ijumaa au kesho Jumamosi.
“Nipo Dar es Salaam kwa mambo yangu binafsi na Jumanne nitajiunga na timu yangu kambini Mbeya, kuhusu habari za Simba na Yanga ukifika muda nitakueleza vizuri lakini sasa nawaza Mbeya City.”
Post a Comment