Kocha Maximo ataka kusajili wawili dirisha dogo


Kocha Mkuu wa Klabu ya Yanga, Mbrazil Marcio Maximo

BOSI wa Ufundi wa Yanga, Marcio Maximo, amesema anataka wachezaji wapya wawili tu anaosema wakitua klabuni hapo tu basi kazi imeisha na ubingwa ataupata kiulaini kabisa, mmoja atakuwa mzawa.
Maximo alisema baada ya kukifanyia tathimini kikosi chake amegundua kwamba amepungukiwa viungo wawili wa kati ambao lazima anunue wapya kwenye dirisha dogo la usajili linaloanza wikiendi ijayo.
Alisema katika mapendekezo yake anataka Kamati ya Usajili ya timu hiyo iliyochini ya Mhandisi Isaac Chanji, Seif Ahmed ‘Seif Magari’, Abdallah Bin Kleb na Mussa Katabaro, kusaka kiungo mmoja mzawa na mwingine wa kigeni huku akigoma kutaja majina yao ingawa Mwanaspoti lina taarifa za awali.
“Ukiangalia timu utaona kwamba hakuna uwiano sawa kati ya viungo na washambuliaji, sasa tuna washambuliaji wengi kuliko viungo hiyo sio sawa sana, tunahitaji kuongeza watu wawili watakaotuongezea nguvu,” alisema Maximo ambaye ameondoka nchini leo sambamba na wachezaji Wabrazili kwenda likizo ya siku 10.
“Nataka wachezaji wawili tu kwa sasa, tayari nimeshawapa majina ya watu ninaowataka, siwezi kukutajia ni nani na nani, lakini tambua kwamba tayari nimeshawasiliana nafikiri mpaka nikirudi baada ya siku 10 naweza kuwakuta hapa,”alisema Maximo.
Wakati Maximo akigoma kuwataja, Mwanaspoti linafahamu kwamba endapo Yanga itamkosa kiungo Jonas Mkude wa Simba itahamishia rada kwa Shaban Nditi wa Mtibwa Sugar.

No comments