Simba yaweka rekodi Dar
SIMBA jana Jumapili iliweka rekodi ya aina yake jijini Dar es Salaam baada ya kushinda mechi yake ya kwanza kati ya saba ilizocheza tangu msimu mpya wa Ligi Kuu Bara uanze.
Bao la Simba lilifungwa na Emmanuel Okwi dakika 77 katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting uliopigwa Uwanja wa Taifa.
Okwi alifunga bao hilo akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Ruvu Shooting Abdallah Rashid kufuatia shuti kali la Elius Maguli.
Mechi hiyo ambayo ilionekana kuwa ya kawaida kwani hakuna timu iliyoonyesha mashambulizi makali langoni kwa wapinzani wake ilimazika Simba ikishinda bao 1-0, ambapo kocha wa Simba Patrick Phiri amesema kwamba kuanza jana ndiyo ulikuwa mwisho wa timu yake kupata matokeo ya sare.
“Najua wana Simba walikuwa wanaumia sana na matokeo ya sare sita mfululizo, huu ndiyo mwisho na sasa ni ushindi tu, nawapongeza wachezaji wangu pamoja na wanachama, mashabiki na viongozi,” alisema.
“Bao alilofunga Okwi lilikuwa zuri ambapo limetengenezwa na watu watatu Amissi Tambwe, Maguli na yeye mwenyewe aliyefanya kazi nzuri ya kufunga.”
Post a Comment