Kiemba aanza kupiga kazi Azam


Amri Kiemba
AMRI Kiemba ataanza mazoezi kwenye kikosi chake kipya cha Azam FC leo Jumatatu, lakini ametoa la moyoni kwa kusema, yaliyomtokea Simba hayamuumizi kichwa na anayachukulia kama sehemu ya changamoto na sasa ametua kwa Bakhresa kila kitu amemwachia Mungu ili aamue hatma yake.
Lakini akaenda mbali na kuwaambia mabosi wake wa sasa, yeye hajui kuchagua, wampe jezi yenye namba yoyote ile iliyopo au watakayoona inamfaa ataivaa.
Kiemba amekwenda Azam kwa mkopo na dau la Sh10 milioni akitokea Simba.
Mchezaji huyo ameliambia Mwanaspoti kuwa: “Tukijaaliwa kesho (leo) nitaanza mazoezi rasmi. Binafsi nimejiandaa vizuri lakini siwezi kutoa ahadi nyingi kila kitu nimemwachia Mungu aamue.”
“Unajua wakati mwingine binadamu tunakosea, unasema nitafanya hiki na hiki lakini utambue kuwa yote yanapangwa na Mungu kikubwa naomba ushirikiano,”alisema Kiemba ambaye amebakiza miezi sita Simba na amekwenda kwa mkopo Azam kwa miezi sita.
“Unaweza kukuta, hata hicho kilichonitokea Simba, ilipangwa tu ili kifanyike hiki kilichofanyika.”
Akizungumzia sakata lake Simba, Kiemba alisema:
“Yote nayachukulia kawaida tu kuwa ni sehemu ya changamoto za maisha, ndivyo ilivyokuwa imepangwa, sitaki kuyazungumzia sana kwa undani.”
Hadi kutua kikosini hapo, Kiemba alikuwa amesimamishwa na uongozi wa Simba kwa kile kinachodaiwa ni utovu wa nidhamu. Alisimamishwa pamoja na wachezaji wenzake, Shaaban Kisiga ‘Marlone’ na Haroun Chanongo.

No comments