Phiri akuna kichwa sakata la Chonongo na Kisiga Simba

Kocha wa Simba, Patrick Phiri, 
KOCHA wa Simba, Patrick Phiri, amesema endapo viongozi wa Simba wataamua kuwarudisha kikosini hapo Haruna Chanongo na Shaban Kisiga waliosimamishwa itamlazimu kutumia muda mwingi kuwajenga kisaikolojia ili warudi katika hali ya mchezo.
Simba iliwasimamisha wachezaji hao watatu baada ya mechi yao dhidi ya Prisons iliyochezwa jijini Mbeya kwa madai ya kucheza chini ya kiwango na utovu wa nidhamu huku kesi zao zikiwa bado zinasikilizwa hadi hivi sasa.
Habari za ndani kutoka Simba zinasema kuwa Kisiga ambaye alisimamishwa kwa kosa la utovu wa nidhamu huenda akasamehewa tofauti na Chanongo anayetuhumiwa kucheza chini ya kiwango na kuhujumu timu katika matokeo yao waliyoyapata kwenye mechi sita za mwanzo, ambazo zilimalizika kwa sare
Phiri aliliambia Mwanaspoti kuwa wachezaji hao ni wazuri lakini suala lao lipo mikononi mwa viongozi ambao wataamua juu ya hatima ya wao kurejea kikosini ama kuenguliwa kabisa.
“Suala la hawa wachezaji lipo chini ya viongozi, ambao wataamua juu yao, ni wachezaji wazuri lakini siwezi kuingilia zaidi ila kama watarejeshwa kikosini nitakuwa na kazi ya ziada ya kuwajenga kisaikolojia ili akili zao zirudi kwenye mchezo,” alisema Phiri ambaye kwa sasa yupo nchini Zambia kwa mapumziko mafupi.
Mbali na hilo Phiri alisema kuwa wachezaji hao wanatakiwa kufahamu kuwa kwenye maisha ya soka kuna vipindi tofauti hivyo kwao wanapita kwenye kipindi kigumu ambacho kinatakiwa kuwajenga na siyo kuwabomoa kwani wanaweza kupotea kwenye soka.

No comments