Simba, Yanga zavizia mastaa 10,TFF yatoa mwongozo
KWA mujibu wa kalenda ya soka ya Tanzania, usajili wa dirisha dogo unaanza leo Jumamosi mpaka Desemba 15.
Mchakato huo unaanza huku wachezaji 10 wa Simba na Yanga mikataba yao ikielekea ukingoni jambo ambalo huenda likanogesha zaidi usajili huo.
Wakati ambapo Azam ikijifanya kama haiwaoni wachezaji hao, Simba na Yanga kila moja inaangalia jinsi inavyoweza kunyakua staa wa mwenzake kati ya hao 10.
Wachezaji 10 wapo sokoni baada ya kubakiza miezi sita katika mikataba yao na kuanzia leo wanaweza kusaini mikataba mipya na klabu yoyote waipendayo na hata kununua sehemu ya mkataba uliobaki na kuondoka.
Kati ya wachezaji hao, kila moja ya klabu hizo inao watano, lakini wapo wengine ambao hadi mapema mwakani watakuwa wamebakiza miezi sita tu katika mikataba yao.
Hii ina maana wachezaji hao wanaruhusiwa kufanya makubaliano na klabu yoyote ile ndani na nje ya nchi ili kujiunga nayo, lakini kwa sharti la kusubiri hadi amalize mkataba wake na klabu anayoichezea sasa.
Hata hivyo njia nyingine nyepesi ya wao kujiunga na timu nyingine ni kuvunja mkataba kwa muda uliobaki wa miezi sita ili waweze kujiunga moja kwa moja na timu mpya walizokubaliana nazo.
Kwa upande wa Yanga wachezaji waliobakiza miezi sita katika mikataba yao ni Haruna Niyonzima, Mrisho Ngassa, Mbuyu Twite, Nizar Khalfan na Hamisi Kiiza wakati kwa upande wa Simba ni Ramadhan Singano ‘Messi’, Said Ndemla, Amissi Tambwe, Haroun Chanongo na William Lucian ‘Gallas’.
Kutwa nzima ya jana Ijumaa Simba ilikuwa na kikao kirefu na kocha wake Patrick Phiri lengo likiwa kupitia taarifa yake ya mechi saba za timu hiyo ilizocheza katika Ligi Kuu Bara na kuambulia pointi tisa, lakini kubwa ikiwa ni usajili wa wachezaji wapya.
Kikao hicho pia kilikuwa kikijadili kuhusu wachezaji waliobakiza muda wa miezi sita katika mikataba yao ambao wanaweza kufanya mazungumzo na timu nyingine. Pia kikao kiliwajadili wachezaji waliosimamishwa na uongozi kwa tuhuma za kuihujumu timu katika matokeo ya sare iliyokuwa ikipata.
Habari kutoka ndani ya Simba zinasema wachezaji ambao wapo katika hali mbaya na huenda wakatolewa kwa mkopo ni Messi na Chanongo kutokana na tuhuma za kuihujumu timu lakini Tambwe anaonekana kuigawa timu kwani baadhi ya viongozi hawamuhitaji huku wachache wakitaka abaki kikosini.
Hali ni nzuri kwa Ndemla na Gallas ambao muda wowote wanaweza kupewa mikataba mipya japokuwa Azam FC wanajitahidi kuzungumza na Ndemla ili wamsajili kwa Sh40 milioni.
Habari zinasema Pierre Kwizera na Raphael Kiongera wameonekana wana matatizo na huenda Pierre akatolewa kwa mkopo nje ya nchi kwa vile mkataba wake ni mrefu, lakini Simba bado wanajadiliana kama wakamtibu Kiongera India au wamteme.
Kwa upande wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Mkurugenzi wa Mashindano, Boniface Wambura aliliambia Mwanaspoti kuwa katika kipindi hiki timu ambazo hazijatimiza idadi ya wachezaji 30 zitakuwa huru kufanya usajili kujazia nafasi zilizowazi.
“Watu wanatakiwa kufuata kanuni za usajili katika wakati huu kwani hiki si kipindi cha kutema wachezaji bila mpangilio, labda kwa makubaliano maalumu tu ila timu ambazo hazijatimiza idadi ya wachezaji 30 zipo huru kujaza nafasi zake,” alisema.
“Halafu kuna wale ambao wamebakiza muda wa miezi sita katika usajili wao, hao wanaruhusiwa kuingia makubaliano mapya na timu nyingine huku wakiendelea kucheza katika klabu zao za sasa na ifahamike wakijisajili kwa njia hiyo siyo kuvunja mkataba.”
Wambura alisema mchezaji aliyebakisha muda wa miezi sita katika mkataba wake ni sawa na yule mwenye mwaka mzima hivyo kuondoka katika timu ni lazima avunje mkataba kwa muda uliobaki kwa mujibu wa kanuni.
Tayari Simba imemwongezea mkataba kiungo wake Jonas Mkude kwa miaka miwili zaidi huku Azam FC ikimsajili beki Serge Wawa kutoka El Merreikh ya Sudan.
Post a Comment