Wanaume vitani tena Ligi Kuu Bara

KIPYENGA cha Ligi Kuu Bara kinatarajiwa
kuanza kupulizwa leo Jumamosi kwenye
viwanja mbalimbali huku jumla ya timu shiriki
12 kati ya 14 zikianza kuuwania ubingwa
unaoshikiliwa na Azam FC.
Msimu uliopita wa ligi , Azam FC walitwaa taji
hilo la ubingwa kwa pointi 62, Yanga 56,
Mbeya City 49 huku wakongwe Simba
wakimaliza wakiwa nafasi ya nne wakiwa na
pointi 38 .
Yanga leo Jumamosi wanatarajiwa kujitupa
kwenye Uwanja wa Jamhuri , Morogoro
kuvaana na wapinzani wao Mtibwa Sugar
wakiwa na benchi jipya la ufundi
litakaloongozwa na Mbrazili , Marcio Maximo
na wasaidizi wake, Leonardo Neiva , Salvatory
Edward , Shadrack Nsajigwa na Juma
Pondamali.
Hicho ndiyo kibarua kigumu cha kwanza kwa
kocha huyo mpya atakachokuwa nacho
ambacho timu hiyo ndani ya misimu mitatu
iliyoshiriki ligi kuu haikuwahi kupata ushindi
zaidi ya sare bao 1- 1.
Awali, kocha huyo aliahidi kuvunja mwiko wa
kuifunga Mtibwa Sugar kwenye uwanja huo.
“Kabla ya kusaini mkataba wa kuifundisha
Yanga, nilipewa baadhi ya ripoti ikiwemo ya
Yanga kushindwa kuifunga Mtibwa Sugar
kwenye Uwanja wa Jamhuri .
“Hivyo nimepanga kuivunja rekodi hiyo kwa
kuwafunga hao Mtibwa Sugar nyumbani
kwao , ninajua kocha wao Maxime ( Mecky )
ananijua vizuri kutokana na kuwahi
kumfundisha nikiwa Stars , ” alisema Maximo .
Katika mechi hiyo , kiungo mshambuliaji mpya
wa timu hiyo , Mbrazili , Andrey Coutinho,
atakosekana kutokana na majeraha ya
kifundo cha mguu na Jerry Tegete
anayeuguza nyonga , wote waliumia kwenye
mechi ya kirafiki dhidi ya Polisi Dar .
Kwa upande wake Maxime alisema kuwa
maandalizi waliyoyafanya na kikosi hicho
yanatosha kupata ushindi kutokana na timu
yake kukamilika kila sehemu .Mechi nyingine
za leo ni Azam FC watakaowakaribisha Polisi
Moro kwenye Uwanja Azam Complex nje
kidogo ya Dar es Salaam.
Nyingine ni Stand United vs Ndanda ( Uwanja
wa Kambarage , Shinyanga ) , Mgambo JKT vs
Kagera Sugar ( Uwanja wa Mkwakwani,
Tanga) , Ruvu Shooting vs Prisons ( Uwanja
wa Mabatini , Pwani) na Mbeya City vs JKT
Ruvu ( Uwanja wa Sokoine, Mbeya) .
Wakongwe Simba wanatarajiwa kujitupa
uwanjani kesho Jumapili kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam kuvaana na Coastal
Union ya mkoani Tanga.Katika mechi hiyo ,
Simba wataivaa Coastal Union wakiwa na
kocha wao mpya Mzambia , Patrick Phiri
aliyeweka rekodi ya kuchukua ubingwa huo
bila kufungwa kwenye msimu wa 2009 /2010 .
Simba msimu huu kikosi chao kimebadilika
kwa kiwango kikubwa kutokana na usajili
walioufanya kwa kumrejesha kiungo
mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi na
Shaabani Kisiga huku wakiwasajili Paul
Kiongera, Pierre Kwizera, Elias Maguli , Joram
Mgeveke, Hussein Sharrifu ‘ Casillas’ na
Manyika Peter Junior.

No comments