Simba inahitaji kuweka vizuri mambo haya ili kukaa sawa



HATIMAYE kocha mpya wa Simba anayetarajiwa kurithi mikoba ya Patrick Phiri amewasili jijini Dar es Salaam jana Jumatano tayari kwa kuanza kazi ya kuinoa timu hiyo.
Kocha huyo, Goran Kopunovic kutoka Serbia anakuwa wa pili kuinoa Simba tangu kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Bara msimu wa 2014-15 baada ya Zdravko Logarusic na Phiri.
Mtihani wa kwanza wa kocha huyo utakuwa ni katika michuano ya Kombe la Mpinduzi inayoanza rasmi leo Alhamisi, Visiwani Zanzibar.
Kuna usemi uliozoeleka kwamba ‘Makocha huajiriwa ili watimuliwe’, usemi huu pamoja na kuwa maarufu lakini si kweli kwamba kila kocha anayeajiriwa lazima atimuliwe bali kuna sababu za msingi za kufanya hivyo.
Sababu kubwa ni matokeo mabaya, timu inapofungwa sana, hoja ya makocha huajiriwa ili watimuliwe inapata nafasi yake.
Hata hivyo kabla ya kutimua kocha ni lazima uongozi utambue majukumu yake kwa timu, kwa maana ya kuwajibika kwa kila jambo muhimu, hiyo ni siri mojawapo inayohalalisha kumtimua au kutomtimua kocha.
Kutokana na hilo ndio maana tunapenda kuukumbusha uongozi wa Simba kwamba kama hawatakaa chini na kuangalia matatizo mengine ya Simba watatimua kila kocha atakayeajiriwa.
Baadhi ya mambo ambayo tumeyaona kuwa ni kiini cha Simba kuyumba hayasababishwi na kocha pekee bali uongozi nao unahusika kwa namna moja au nyingine.
Upo ukweli kwamba kwa sasa Simba hakuna umoja, jambo baya ni kwamba umoja huo umekosekana zaidi kwa wachezaji ambao ndio wahusika wakuu wa mafanikio ya Simba.
Kukosekana kwa umoja kunachangiwa na uongozi ambao umeshindwa kuwatendea haki sawa wachezaji wote, badala yake kumekuwa na ubaguzi wa hali ya juu.
Usawa tunaouzungumzia hapa si katika maslahi ya mchezaji mmoja mmoja kwamba wachezaji walipwe mishahara sawa, hapana zama hizo zilishapita. Usawa tunaouzungumzia ni katika mambo mengine.
Mfano hivi karibuni tumesikia kwamba kuna kundi la wachezaji wa Simba waliosafiri kwa ndege kutoka Zanzibar na wengine wakapanda boti.

No comments