
KIKOSI kamili cha Yanga leo Alhamisi kinaondoka kwa boti kwenda visiwani Zanzibar kushiriki Kombe la Mapinduzi, lakini kocha wa timu hiyo, Hans Van Der Pluijm amefanya marekebisho kadhaa katika kikosi chake na kukiongezea mbinu za ushindi ili kitwae ubingwa.
Yanga imepangwa Kundi A na timu za SC Villa ya Uganda, Polisi na Shaba zote za Zanzibar. Jangwani wataanza harakati zao za kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, keshokutwa Jumamosi watakapocheza na SC Villa katika Uwanja wa Amaan.
Pluijm anataka kuitumia michuano hiyo inayoanza leo Januari Mosi, kutazama jinsi marekebisho aliyofanya baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Azam FC katika Ligi Kuu Bara yanavyofanikiwa.
Kwa miaka miwili iliyopita, Yanga haikushiriki michuano hiyo maalumu kuadhimisha sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na sababu mbalimbali, lakini sasa imeingiza timu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pluijm raia wa Uholanzi alisema anataka kushiriki michuano hiyo kikamilifu na kuiwezesha Yanga kutwaa ubingwa ndiyo maana amefanya marekebisho kadhaa kikosini kumweka vizuri kila mchezaji.
Pluijm ambaye keshokutwa Jumamosi atakuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa, alisema tayari ameshawapa mbinu wachezaji ambapo kila mmoja anatakiwa kukaba kwa nguvu huku na kuanzisha mashambulizi kwa kutumia mabeki wa pembeni na mawinga wao.
“Mchezo na Azam timu ilionekana kutokuwa katika kukaba, nimewafundisha namna ya kuzuia kwa mbinu, halafu nataka washambulie kwa kutumia mawinga na mabeki wa pembeni ambao watakuwa wanabadilishana kwa kadiri muda unavyokwenda,” alisema.
“Tutacheza kwa kasi zaidi ya tulivyocheza na Azam kwani tutaweza kuwachanganya wapinzani wetu watakaocheza soka la taratibu, nimeambiwa umuhimu wa michuano hii na sitaki kudharau kitu nataka kwenda kushindana siyo kushangaa visiwa, nimewaambia hivyo hata wachezaji wangu.”
Katika kuonyesha ipo makini na michuano hiyo, Yanga imeongeza wachezaji watano zaidi ya wale 25 watakaogharimiwa na waandaaji wa michuano hiyo hivyo uongozi umekubali kuwalipia wachezaji walioongezeka kwenye msafara.
Post a Comment