Mserbia atakutana na changamoto hizi ndani ya Simba


SIMBA ipo katika mchakato wa kubadili kocha ili kuinusuru timu hiyo na matokeo yasiyoridhisha katika Ligi Kuu Bara na tayari Kocha Goran Kapunovic ameshawasili nchini kuchukua mikoba ya kuifundisha timu hiyo kutoka kwa Mzambia Patrick Phiri.
Kama ilivyo kwa Phiri, Kapunovic raia wa Serbia ana changamoto kubwa ya kuhakikisha Simba inafanya vizuri katika ligi na mtihani wake wa kwanza unaweza kuwa leo Alhamisi dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Kombe la Mapinduzi.
Simba inacheza na Mtibwa leo usiku kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja, Zanzibar katika mechi za ufunguzi za michuano hiyo maalumu ya kuelekea sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.
Ujio wa Kapunovic unakuja baada ya Simba kucheza mechi nane za ligi kuu ambapo imetoa sare sita, ikapoteza mechi moja na imeshinda moja, hivyo kushika nafasi ya kumi ikiwa na pointi tisa tu, ndipo uongozi ulipoona haja ya kumleta kocha huyo achukue nafasi ya Phiri.
Kapunovic aliwasili jana Jumatano saa 1:30 asubuhi kwa Ndege ya Qatar na kupokewa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Collins Frisch akiwa na Katibu Mkuu wakeo, Steven Ally.
Muda mfupi baada ya kuwasili, Kapunovic aliliambia Mwanaspoti kuwa amekuja kuipa mafanikio Simba ambayo anaamini ni timu kubwa Afrika kwani muda mrefu imekuwa ikihangaika kupata ushindi hasa katika mechi za ligi.
Alisema anakuja Simba na kiu kubwa ya kutaka kuipa mafanikio timu hiyo huku pia akieleza wazi kwamba atatumia soka lake la kushambulia kwa nguvu likiambatana na nidhamu, uwajibikaji na heshima kwani ndiyo vitu vitakavyosaidia kupatikana pointi tatu kwenye kila mechi.
“Siku zote maisha yangu ni soka, sitaki mchezo katika hilo. Kikubwa ninataka kuona timu ninayoifundisha inafanikiwa, nina taarifa nyingi kuhusu wachezaji wa hapa, lakini pia nimeambiwa kwamba hapa unahitajika ushindi nipo tayari kwa kazi kama tukikubaliana na uongozi,”alisema Kapunovic.
Muda mfupi baada ya kutua nchini, Kapunovic alikwenda kukutana na viongozi wa Simba ili kukubaliana baadhi ya mambo ya mkataba halafu ikiwezekana jioni au leo asubuhi aende Zanzibar kuungana na kikosi cha timu hiyo katika Kombe la Mapinduzi.
Naye Kocha Jean Marie Ntagwabira raia wa Rwanda anayetajwa kupewa kazi ya Kocha Msaidizi aliliambia Mwanaspoti kutoka Kigali, akisema: “Nimeshaongea na Simba na nipo tayari kufanya kazi na Kapunovic kwani namjua, nasubiri simu ya Simba ili tufikie makubaliano.”
PHIRI AOMBA LIKIZO, PLUIJM ASIKITIKA
Wakati Kapunovic akiwasili nchini, Kocha Phiri ambaye hakuwa ametamkiwa kuhusu kutimuliwa kwake hadi jana asubuhi, aliuomba uongozi wa Simba umpe ruhusa ya siku chache ili akapumzike kwao Zambia.

No comments