Wachezaji hawa walalamikia Mishahara Simba


NI baadhi tu ya wachezaji ndio waliolipwa mishahara yao katika klabu ya Simba huku wengine wakisotea mishahara kwa miezi miwili licha ya mdhamini wao Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kuilipa klabu hiyo mishahara yote.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wachezaji walisema wanadai mishahara ya miezi miwili huku kukiwa hakuna ufafanuzi wowote kutoka kwa uongozi na zipo taarifa zinazoeleza wapo waliolipwa mwezi mmoja na wengine hawadai kabisa.
Wachezaji hao walithibitisha kuwepo kwa tatizo hilo ndani ya timu na kwenda mbali zaidi kwa kusema linaongeza hali ya matabaka ndani ya timu na endapo uongozi utaendelea kuwa kimya mambo yatazidi kuwa mabaya uwanjani.
“Unajua baadhi hatujalipwa mishahara mpaka sasa na hatujaambiwa kitu ila tunasikia kuna wenzetu wamelipwa, sasa hatujui wanaangalia vigezo gani, maana kama ni kazi wote tunafanya iweje wengine walipwe na wengine wasilipwe? Hatutendewi haki,” alisema mmoja wa wachezaji hao.
Chanzo cha habari kutoka Simba kilisema hali ya fedha ndani ya klabu hiyo imekuwa mbaya kwa sasa kwani timu haina fedha na viongozi wanasubiri zawadi ya Sh92 milioni ya Nani Mtani Jembe waliyoshinda kwa kuizidi Yanga ili warekebishe baadhi ya mambo yaliyokwama.
“Nafikiri kuna matumizi yanayofanyika ambayo hayana ulazima katika klabu yetu, iweje wengine walipwe mishahara na wengine wasilipwe? Hii siyo sahihi kwani inaleta makundi, wachezaji wanatakiwa kuwa na thamani sawa, TBL wanatoa fedha hata kama haitoshi wanashindwaje kutafuta fedha ya kuongezea?” Alihoji mmoja wa wachezaji hao.
“Fedha za mgawo wa mechi ya Nani Mtani Jembe, wachezaji wanalalamika mpaka sasa kuna baadhi wamelipwa Sh2 milioni, staa mmoja tu wa hapa (anataja jina) ndiye kalipwa Sh1 milioni, wengine wamepewa Sh100,000, 200,000 na 600,000 kweli hapo kuna usawa?”
Alipoulizwa Katibu Mkuu wa Simba, Steven Ally alisema: “Sina taarifa za mchezaji ambaye hajalipwa mshahara, hata Rais (Evans Aveva) taarifa hizo hazijui, nani huyo ambaye hajalipwa?”
Kiongozi mmoja kutoka TBL alisema, hakuna mwezi ambao wamepitisha bila kuingiza fedha katika klabu zote mbili wanazozidhamini Simba na Yanga kwa ajili ya kulipa mishahara.
Kuthibitisha hilo, Mwanaspoti lilimtafuta Meneja wa Bia ya Kilimanjaro inayodhamini timu hizo, Pamera Kikuli, ambaye alisema: “Kama fedha za mishahara tumeshawalipa Simba na Yanga isipokuwa za Nani Mtani Jembe ndizo hazijalipwa peke yake kwani kuna taratibu zilichelewa kufanywa.”
Katika Mtani Jembe, Simba iliifunga Yanga mabao 2-0 na kunyakua Sh 15 milioni huku ikipata Sh 77 milioni ambazo zilitokana na utumaji wa ujumbe mfupi kwa njia ya simu uliokuwa unatumwa na mashabikli wake, hivyo kuondoka na jumla ya Sh 92 milioni.
Hii ni mara ya pili Simba kutamba mechi hiyo.

No comments