
YANGA ambayo kesho Jumapili itacheza na Azam FC mchezo wa Ligi Kuu Bara, imeshtukia mchezo wa baadhi ya wachezaji wake wanaokaa benchi kwa muda mrefu na kuna mkakati unaoandaliwa ili kukomesha hali hiyo.
Kati ya mambo yatakayofanyiwa kazi na Katibu Mkuu mpya wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha ni kuhakikisha kikosi hicho kinaondokana na wachezaji wanaokaa benchi bila sababu ya msingi huku wakichota fedha za bure klabuni hapo.
Kauli hiyo ya katibu ni kama uchokozi kwa kipa wa timu hiyo Ally Mustapha ‘Barthez’ na straika Jerry Tegete ambao wamekuwa wakisugua benchi kwa muda mrefu sasa bila kupata uhakika wa namba kwenye kikosi cha kwanza.
Katibu huyo alisema ni bora kuwa na wachezaji wachache lakini wanaoweza kuleta maendeleo ya timu kuliko timu hiyo kuendelea kuwa na idadi kubwa ya wachezaji ambao wanachukua fedha nyingi bila kufanya kazi.
“Ni kweli tunahitaji Yanga iwe na wachezaji wenye ushindani wa hali ya juu, lakini ambao watakuwa wanacheza na siyo kusugua benchi huku wakiwa wanalipwa mishahara ambayo tungeweza kufanyia kazi nyingine,” alisema.
Katibu huyo alisema anataka kusimamia suala la uvumbuzi wa vipaji vya vijana wakataowajumuisha kwenye kikosi cha timu yao ya vijana ili kupunguza gharama za usajili kwa siku za usoni.
“Kwa mfano tukiamua kufanya ufuatiliaji wa wachezaji wa mtaani ni rahisi wakaanzia timu B, baada ya kupata uzoefu wakacheza timu ya wakubwa, hilo litapunguza gharama kubwa inayotumika kusajili wachezaji mwisho wa siku wanaishia kukalia benchi,” alisema.
Tiboroha ambaye ni msomi wa ngazi ya Udaktari amerithi mikoba ya Beno Njovu aliyeondoka Yanga mwezi uliopita baada ya kumalizika kwa mkataba wake.
Post a Comment