Hizi ni rekodi za Yanga Vs Azam.. Yanga ni baba lao tu

Match Preview: Azam- Yanga , Wenyeji kulipa kisasi

Azam ambao ndiyo wenyeji katika mchezo huo wa kesho wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kufungwa mabao 3-0, na Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii
MABINGWA watetezi wa Ligi ya Vodacom Tanzania bara Azam kesho wanashuka kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaam kukabiliana na Yanga inayonolewa na kocha mpya raia wa Uholanzi Hans van der Pluijm.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kutokana na timu hizo kuwa na ushindani mkubwa katika siku za karibuni ikiwemo msimu uliopita kukimbizana hadi dakika za mwisho kuwania ubingwa ambao ulitua Azam kwa tofauti ya pointi nne.
Azam ambao ndiyo wenyeji katika mchezo huo wa kesho wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kufungwa mabao 3-0, na Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii uliofanyika kwenye uwanja huo Septemba 14.
Kipigo hicho bado kipo kwenye vichwa vya wachezaji wa Azam pamoja na benchi lake la ufundi lililopo chini ya kocha Mcameroon, Joseph Omog na msaidizi wake George Nsimbe ‘Best’ aliyejiunga na timu hiyo wiki tatu zilizopita kuchukua nafasi ya Kalimangonga Ongalla.
Azam itaingia katika mchezo wa kesho ikiwa inajivunia usajili iliyoufanya kwenye dirisha dogo kwa kuwasajili Amri Kiemba, Serge Wawa na Brian Majwega ambao bila shaka wataanzishwa kwenye pambano la kesho ili kuipa ushindi timu hiyo iliyopania kutetea ubingwa wake kwa mara ya pili.
Kwamtazamo wa timu zote mbili Azam inaonekana imejipanga na imedhamiria kushinda mchezo wa kesho kwa kutumia rasilimali ya kikosi kipana ilichonacho ili kuongeza machungu kwa wapinzani wao Yanga ambao wiki mbili zilizopita walifungwa mabao 2-0, na wapinzani wao Simba na kumtimua kocha wao Mbrazili Marcio Maximo.
Azam iliyopoteza mechi mbili kati ya saba za ligi ilizocheza msimu huu hivi karibuni iliweka kambi ya siku 10 nchini Uganda kujiandaa na pambano hilo nia na madhumuni yao ikiwa ni kuhakikisha wanaifunga Yanga na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao.
Lakini wakati Azam wanajipanga kwa ajili ya pambano hilo Yanga nao hawajalala wapo katika mawindo makali kwenye viwanja wa Boko Veterani wakijifua kuhakikisha wanapoza machungu ya mabao 2-0 kutoka kwa wapinzani wao Simba.
Licha ya kuwa na benchi jipya la ufundi pia Yanga kama ilivyo kwa Azam imeongeza wachezaji watatu wapya kwenye dirisha dogo ili kuimarisha kikosi chake lengo likiwa ni kurdisha ubingwa wao wa Vodacom ambao msimu uliopita ulichukiliwa na Azam.
Yanga imemsajili shambuliaji kutoka Liberia Kpah Sean Sherman kutoka Citinkaya TSK ya Cyprus Kaskazini Amisi Tambwe aliyekuwa akiichezea Simba na mzalendo Dany Mrwanda, aliyekuwa akiichezea Polisi Moro.
Kwa usajili huu Yanga inaonekana kuwa na safu kali ya ushambuliaji hivyo niwazi mabeki wa timu pinzani wakiwemo wa Azam hawatakiwa kufanya makosa ya kizembe kwani wachezaji hao ni hatari sana kila wanapopata nafasi.
Yanga imekuwa na rekodi nzuri inapokutana na Azam kutokana na ukongwe iliyokuwa nao lakini katika pambano hili chochote kinaweza kutokea kutokana na uimara wa timu zote mbili ambazo ndizo zitakazo iwakilisha Tanzania katika michuano ya kimataifa mwaka 2015.
Hans Pluijm aliyepewa mikoba ya Maximo atakuwa kwenye benchi la Yanga akitaka kuwaliwaza mashabiki wa timu hiyo ambao walikosa raha siku za karibuni kutokana na kuzomewa na wenzao wa Simba kufuatia kipigo hicho cha 2-0.
Japo mashabiki wa Yanga wameanza kutembea kwa amani baada ya Simba kufungwa na Kagera Sugar Ijumaa lakini itapendeza zaidi kama timu yao itapata ushindi mbele ya Azam ambayo kwa sasa inaaminika ndiyo timu ngumu na bora kwenye ligi yaTanzania.
Msimu uliopita katika mechi mbili za ligi Azam ilivuna pointi nne kutoka kwa Yanga baada ya kushinda mchezo wa kwanza mabao 3-2 na katika mchezo wa marudiano uliofanyika Machi timu hizo zilikwenda sare ya 1-1

No comments