
KWELI Kagera Sugar ni kiboko ya vigogo kwani jana Ijumaa imeendeleza rekodi yake kwa kuifunga Simba bao 1-0 baada ya kuifunga Yanga kwa matokeo kama hayo Novemba Mosi, mwaka huu mjini Bukoba.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Kagera ilipata bao lake dakika ya 21 lililofungwa na Atupele Green.
Green ambaye aliwahi kuzichezea Yanga na Coastal Union ya Tanga, aliifungia Kagera bao hilo akiunganisha kwa kichwa mpira uliorushwa na beki wake Abou Mtiro ambao kipa wa Simba, Ivo Mapunda alishindwa kuuokoa.
Matokeo hayo yameifanya Kagera kufikisha pointi 13 na kujikita nafasi ya nne wakati Simba imebaki nafasi ya saba ikiwa na pointi zake tisa.
Kocha wa Simba, Patrick Phiri aliwaanzisha wachezaji wake wapya Dan na Simon Sserunkuma pamoja na beki Juuko Murshid hata hivyo hawakuweza kuizidi Kagera iliyokuwa ikicheza kwa kutulia muda mwingi wa mchezo huo.
Simba iilikosa mabao ya wazi kwenye dakika ya 23 kupitia kwa Simon Sserunkuma na dakika ya 43 na 82 pale nahodha wake, Emmanuel Okwi alipopiga mpira nje kidogo ya lango.
Phiri alifanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kuwatoa Ramadhani Singano, Dan Sserunkuma na Awadhi Juma na kuwaingiza Elius Maguli, Shaaban Kisiga ‘Marlone’ na Said Ndemla. Huo ni mchezo wa nane kwa Simba ambapo imeambulia sare sita huku ikishinda mechi moja na kufungwa mara moja.
Kagera Sugar ilimtoa Benjamin Asukile na kumwingiza Victor Hussein na Babu Ally aliyeumia dakika ya 88, Simon Lucas aliingia.
Simba: Mapunda, Hassan Kessy, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Singano/Maguli, Awadhi/Kisiga, Dan/Ndemla, Simon, Okwi
Kagera: Agatony Anthony, Salum Kanoni, Aboubakari Mtiro, Erick Kyaruz, George Kavila, Malegeres Mwangwa, Paul Ngwai, Babu/Lucas, Atupele Green, Daud Jumanne, Asukile/Hussein.
Post a Comment