Kocha Azam aibipu Yanga.. Soma alichokisema

HAMTUWEZI ndiyo kauli ya kila kocha ambaye timu yake wikiendi hii inashuka uwanjani kucheza mechi za raundi ya nane za mwendelezo wa Ligi Kuu Bara.
Baada ya mapumziko ya mwezi mmoja na nusu, Simba na Kagera Sugra ndizo zilizoanza kurejea uwanjani ambapo jana Ijumaa zilicheza jijini Dar es Salaam.
Kabla ya mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Simba ilikuwa imeweka kambi yake Zanzibar wakati Kagera yenyewe iliwahi kutoka Bukoba kuja Dar es Salaam mapema wiki hii na kuendelea na maandalizi mengine.
Licha ya kuwepo kwa mechi kadhaa za ligi hiyo leo Jumamosi na kesho Jumapili, mechi ya kesho kati ya Azam FC na Yanga ndiyo iliyoteka hisia za mashabiki wengi kwani inaonekana kutawaliwa na ubabe kutoka kwa kila timu. Timu hizo zinarejea uwanjani baada ya mapumziko hayo ambayo yaliwekwa maalumu kutoa mwanya wa timu kusajili na kupisha kufanyika kwa michuano ya Kombe la Chalenji na Kombe la Uhai. Hata hivyo, michuano yote hiyo haikufanyika.
Yanga itaingia uwanjani ikiwa na kocha mpya Hans Van Der Pluijm raia wa Uholanzi aliyepewa kazi baada ya Mbrazili Marcio kusitishiwa mkataba wake akiwa ameiongoza timu yake katika mechi saba za awali.
Timu hizo zinaingia uwanjani zote zikiwa na pointi 13, lakini Yanga inashika nafasi ya pili kutokana na kuizidi Azam mabao ya kufunga ikiwa imefunga mabao tisa huku wapinzani wao wakiwa na mabao nane na wanashika nafasi ya tatu. Mtibwa Sugar ipo kileleni ikiwa na pointi 15.
Vikosi vyote vimejitahidi kufanya usajili wa maana wakati wa dirisha dogo la usajili ambapo Yanga imesajili wachezaji wanne ambao ni mastraika Amissi Tambwe raia wa Burundi aliyeachwa na Simba , Danny Mrwanda (Polisi Moro), Kpah Sherman (Aries FC- Liberia) na kipa Alphonce Majogo kutoka Friends Rangers. Azam yenyewe imewasajili beki Paschal Wawa raia wa Ivory Coast, winga Brian Mwajega kutoka KCCA na kiungo Amri Kiemba aliyesajiliwa kwa mkopo kutoka Simba.
Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 3-0 mbele ya Azam kwenye mechi ya Ngao ya Hisani iliyochezwa Septemba 13, mwaka huu kukaribisha msimu huu wa ligi
Kocha Pluijm aliliambia Mwanaspoti, endapo wachezaji wote watatimiza wajibu wao kwenye mchezo huo wa kesho watakuwa na nafasi kubwa ya ushindi licha ya ukweli kwamba Azam ni timu nzuri na itatoa upinzani mkali.
“Naiheshimu Azam kwani ni timu nzuri, tunakwenda uwanjani kupambana licha ya kwamba nimekaa na timu kwa siku chache lakini kila mchezaji ameonekana kuwa na morali ya juu kwenye kupambana, kila mchezaji anatamani kushinde mchezo huo,” alisema Pluijm
Kocha msaidizi wa Azam, Ibrahim Shikanda alisema; “Tumejiandaa vema kuelekea mchezo huo hasa ukizingatia tuliweka kambi nchini Uganda na kucheza michezo kadhaa ya kirafiki, tumepanga pia kuwatumia washambuliaji wetu Didier Kavumbagu na Kipre Tchetche kuiongoza safu ya ushambuliaji na tunaimani watafanya kazi nzuri.”
Mechi nyingine zitakazochezwa kesho Jumapili ni kati ya Mbeya City na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Mbeya City inashika mkia katika ligi ikiwa na pointi tano tu ikifuatiwa na Ndanda yenye pointi sita, hivyo mechi yao itakuwa kali kwa kila timu ikitaka kuondoka mkiani.

No comments