
YANGA imepangwa kucheza na Botswana Defence Force (BDF) katika mechi yake ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kocha wa timu hiyo, Hans Van Der Pluijm ametamka kuwa amepata taarifa za awali kuhusu wapinzani wao na amepanga kuwavamia kwa kutuma mtu wa kuipeleleza zaidi timu hiyo.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeipanga kucheza na BDF inayomilikiwa na Jeshi la Botswana kati ya Februari 12 na 15 mwakani jijini Dar es Salaam kisha kurudiana kati ya Februari 27 na Machi Mosi huko Botswana.
Pluijm aliliambia Mwanaspoti kuwa muda mfupi baada ya CAF kutoa ratiba hiyo mapema wiki hii, alipata taarifa fupi kuhusu wapinzani wao na kukiri kuwa timu ya kawaida kupambana nayo lakini akasema katika soka lolote laweza kutokea hivyo atamtuma msaidizi wake Boniface Mkwasa akawatazame kwa undani.
Kocha huyo mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika soka la Afrika, alisema katika maisha yake hajawahi kuiogopa timu yoyote pinzani anayokutana nayo, hivyo anaiheshimu BDF kwani ni mabingwa wa nchi yao hivyo si timu itakayomfanya ajisahau kufanya maandalizi ya kutosha.
“Nimefanikiwa kupata taarifa za awali kuhusu BDF, lakini ili kukamilisha kazi yangu napanga mkakati wa kumtuma Mkwasa Botswana kuweza kuwaona kwa macho BDF kabla ya kuwasukia mpango wa kuwang’oa,” alisema Pluijm ambaye kikosi chake kina straika Kpah Sherman.
“Hizo taarifa za awali kuhusu BDF si mbaya sana, kwani zimenipa mwanga wa kuifahamu timu hiyo vizuri lakini nikifanikiwa kumpeleka msaidizi wangu mambo yatakuwa mazuri zaidi. Lakini kama mambo yakiwa mazuri zaidi nitakwenda mwenyewe kuisoma BDF.”
Kocha huyo aliwahi kumtuma Mkwasa nchini Misri kwa kazi ya kwenda kuwasoma Al Ahly ya huko mwaka huu ambapo matunda yake yalionekana baada ya Yanga kushinda bao 1-0 katika mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam lakini ikafungwa katika marudiano jijini la Alexandria, Misri na kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CAF, Azam imepangwa kuanza na El Merreikh ya Sudan katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika kujiandaa na mchezo huo, Azam kupitia kwa Afisa Mtendaji Mkuu wake, Saad Kawemba, imesema imepanga kutuma watu wake Sudan ili kuipeleleza El Merreikh.
“Tumeiona ratiba iliyopangwa na CAF, wapinzani wetu ni moja kati ya timu kali hivyo hatutolala katika maandalizi,” alisema Kawemba.
“Tutatuma watu kuitazama El Merreikh ilivyo kwa sasa ili tuijue vizuri.”
Kwa upande wa Zanzibar, Polisi itacheza na CF Mounana ya Gabon katika Kombe la Shirikisho huku KMKM ikipangiwa kucheza na Al Hilal ya Sudan katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Post a Comment