Ushauri wa Cannavaro kuelekea mechi dhidi ya Azam

NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro, hataweza kuiongoza timu yake keshokutwa Jumapili dhidi ya Azam FC, lakini
amewapa mbinu mabeki wenzake za kuwazuia washambuliaji; Didier Kavumbagu na Kipre Tchetche kisha akasema: “Kama mkiwazuia hao, mnaifunga Azam.”
Cannavaro yupo katika kikosi cha Yanga, lakini hatocheza mechi dhidi ya Azam kwani anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa katika mchezo na Kagera Sugar uliochezwa Novemba Mosi kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba ambapo Yanga ilifungwa bao 1-0.
Tayari beki huyo amekosa mechi moja dhidi ya Mgambo JKT ambayo ilichezwa Novemba 8 Uwanja wa Taifa ambayo Yanga ilishinda mabao 2-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Cannavaro anayecheza beki ya kati alisema ingawa hatokuwepo katika mechi hiyo, mabeki wa pembeni wa timu yake wanatakiwa kuwa makini na kasi ya Tchetche ambaye mara nyingi hupenda kutokea pembeni kutengeneza mashambulizi ya maana.
Alisema wakati mabeki wa pembeni wakifanya kazi hiyo ikiwa ni pamoja na kumzuia winga mpya wa Azam, Brian Majwega aliyesajiliwa kutoka KCCA ya Uganda, pia mabeki wa kati ambao ni Kelvin Yondani na Mbuyu Twite anayechukua nafasi yake wanatakiwa kufanya kazi ya kuhakikisha Kavumbagu hapati nafasi ya kulisogelea eneo la lao la hatari kwani ni hatari sana kwao.
“Kavumbagu ni mzuri katika kuchagua wapi kwa kupiga na akipewa nafasi ya kujitawala katika eneo hilo anaweza kusababisha matatizo makubwa, hivyo wanatakiwa kumalizana naye akiwa mbali na eneo hilo kwani hata mkiwa sita mnaweza msimpokonye mpira mguuni,” alisema. “Nakuhakikishia kama mabeki wenzangu wakiwazuia ipasavyo Tchetche na Kavumbagu basi Azam watafungika kirahisi Jumapili.”

No comments