Emmanuel Okwi ndani ya Simba SC
Simba inatarajia kuvunja benki kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili ili kuipata saini ya mshambuliaji wake wa zamani raia wa Uganda Emmanuel Okwi
Klabu ya Simba inatarajia kuvunja benki kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili kwa kutoa kiasi cha dola 120,000 kwa timu ya Sonderjiske ya Denmark ili kuipata saini ya mshambuliaji wake wa zamani raia wa Uganda Emmanuel Okwi.
Mwenyeki wa Kamati ya Usajili wa klabu ya Simba Zacharia Hans Poppe, ameiambia Goal, wanapambana na wenzake kuhakikisha wanatoa pesa hizo ili kumrudisha msimbazi mshambuliaji huyo aliyefanya vizuri katika vipindi vyote viwili alivyoichezea timu hiyo.
“Tumepanga kulipa pesa hizo kwa klabu yake ya Sonderjiske ili kumpata angalau kwa msimu mmoja, na kama tutafuraishwa na kiwango chake tutamuongeza mkataba mwingine,”amesema Hans Poppe.
Kiongozi huyo amesema wamegundua timu yao pamoja na kufanya vizuri kwenye mzunguko wa kwanza lakini bado wana tatizo la winga na suluhisho kubwa wameona ni Okwi.
Amesema sababu ya kumpendekeza Okwi ni kutokana na kuijua vizuri ligi ya Tanzania kutokana na kucheza kwa misimu mitano akiwa na klabu yao na wapinzani wao Yanga.
“Pia anauzoefu mkubwa na michuano ya kimataifa na ukiangalia kasi yetu tuna uhakika msimu huu tukapata moja ya nafasi za kushiriki michuano ya kimataifa ndiyo maana kocha wetu pia ametushauri kuanza harakati za kusajili wachezaji wenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa,”amesema.
Hans Poppe amesema kwasasa wapo katika mazungumzo na uongozi wa timu hiyo anayochezea Mganda huyo na mambo yakikamilika mchezaji huyo anaweza kutua kabla ja mwezi Januari na kuanza kuichezea Simba.
Endapo Okwi atatua Msimbazi msimu huu huenda akavunja ufalme wa Shizza Kichuyaambaye ndiye anayetumia jezi namba 25, ilikuwa ikivaliwa na Okwi na kupata nayo mafanikio makubwa kama ilivyo kwa Kichuaya hivisasa.
Post a Comment