Tshabalala tisha mbaya
BEKI wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, ametajwa na makocha wengi wa kigeni kuwa ni bonge la mchezaji.
Kocha wa viungo wa Simba, Mserbia Dusan Macmilovic amemsifu Tshabalala akisema, ni miongoni mwa wachezaji bora Simba.
“Kuna vitu vidogo ambavyo Tshabalala anahitaji kufanya ili awe mchezaji ambaye anaweza kucheza Ulaya. Kwa hapa Tanzania ni wazi tayari yupo kwenye kiwango cha juu,” alisema.
“Umri wake unamruhusu na akizingatia mambo machache ya kiufundi haswa ya kupandisha mashambulizi, basi ataweza kuwa tishio sana,” alisifu kocha huyo.
Mwaka jana aliyekuwa kocha wa Simba, Patrick Phiri, aliwahi kusema wazi kuwa Tshabalala ni mchezaji mdogo, lakini mwenye uwezo wa mchezaji mzoefu pia alikuwa akimsifu kwa kupenda kujituma zaidi.
Naye kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm mwishoni mwa msimu uliopita alimtaja Tshabalala kama beki bora wa kushoto wa Ligi Kuu.
Alisema: “Hakuna beki wa pembeni aliyemzidi Tshabalala kwa msimu uliopita. Yupo makini na ndiye mchezaji wangu bora kwenye nafasi za mabeki wa pembeni Ligi kuu Bara.”
Alipokuja Kocha Mserbia Goran Kopunovic naye alimnyooshea kidole Tshabalala akisema: “Ni mchezaji ambaye nikiwa pamoja na wachezaji wengine wa aina yake nitachukua Ligi kirahisi msimu ujao.”
Kocha huyo akafafanua kuwa Tshabalala ni mchezaji anayejitambua na kujituma kwenye kila kitu na haikuwa ajabu mwishoni mwa msimu aliteuliwa kuwa mmoja wa waliokuwa wakiwania Tuzo ya Mchezaji Bora ambayo hata hivyo ilienda kwa Simon Msuva wa Yanga
Post a Comment