Mkude, Kiiza wafunguka tena Msimbazi
KIUNGO mkabaji wa Simba, Jonas Mkude ameupongeza uongozi wa Simba kwa kumrejesha Mwinyi Kazimoto akisema atarejesha ufalme wa klabu yao Bara.
Mkude alisema: “Tulikosa kiungo mzoefu na mwenye uwezo kama wa Kazimoto, ni muda wetu sasa kulitawala soka la Tanzania. Nimesikia juu ya ujio wa Kazimoto, bado sijamuona kambini lakini kama kuna kitu kikubwa walichofanya uongozi ni kumrudisha fundi Kazimoto.
“Tangu alivyoondoka, sikuona aliyeweza kufunika kazi yake, mimi binafsi naamini sijaweza kuufikia ubora wake, lakini sasa naamini anakuja na vitu vipya ukizingatia kuwa ana uzoefu mkubwa na amecheza soka nje.
“Hivi karibuni nilicheza naye kwenye Taifa Stars, kiukweli yuko vizuri sana hata kuliko vile alivyokuwa kabla ya kuondoka Simba.”
Kiungo huyo pia amebainisha kuwa kwa usajili uliofanywa msimu huu ni lazima kila mchezaji ajitume ili ajihakikishie namba.
“Usiwaone akina Kiiza (Hamis), Mgosi (Mussa Hassan) na wengine wote wageni, wako vizuri sema tu kwa sasa mchezaji kupata nafasi kwenye kikosi ni rahisi na hauhitaji kutumia nguvu nyingi kama ilivyokuwa hapo nyuma wakati timu ilipokuwa na viungo kama kina Kazimoto, Haruna Moshi ‘Boban’ na marehemu Mafisango (Mutesa).
Kiiza
Mshambuliaji Hamis Kiiza amekiri kinachofanywa na Simba kwa sasa hakuwahi kukiona hata Yanga na kudai kuwa uwepo wa kocha wa viungo Simba utafanya kila mchezaji awe staa kwani kila mmoja lazima awe na kiwango bora.
Kiiza ambaye ni raia wa Uganda alisema: “Nisikufiche, nilivyokuwa Yanga kilichonipa umaarufu ni uwezo wangu na kujituma kwangu lakini uwezo wangu mkubwa ulichangiwa na kocha wa viungo.
“ Pale Yanga hakukuwa na kocha wa viungo ingawa mimi binafsi nilikuwa na kocha wangu ambaye nilikuwa nikimlipa mwenyewe ili niwe fiti na hicho ndicho kilichonijengea jina.
“Kwa hali hii ya Simba naamini sasa kila mchezaji atakuwa staa na atakuwa na jina kubwa kutokana na uwezo atakaokuwa nao uwanjani.
“Kama kuna kitu Simba itakuwa imezipiga bao klabu zingine kwanza ni kuwa na mtaalamu wa viungo lakini pia itakuwa na wachezaji wengi wenye uwezo wa ajabu.
Post a Comment