Huyu jamaa ni jembe la ukweli...
LICHA ya kikosi chao kusheheni mafundi kadhaa wa soka. Klabu ya Azam ni kama haijaridhika hasa baada ya kuamua kumsainisha kiungo mahiri na nahodha msaidizi wa timu ya taifa ya Rwanda, Jean Baptiste Mugiraneza maarufu kwa jina la Migi.
Kiungo huyo ametua Azam kwa mkataba wa miaka miwili na tayari ameshaanza kuonyesha makali yake kwenye michuano ya Kombe la Kagame ambalo amelichezea baada ya klabu yake ya awali ya APR ya Rwanda kumruhusu kukipiga kwa ‘Wanalambalamba’.
Mkali huyo amepata wasaa wa kuteta na Mwanaspoti na jambo la kwanza ambalo alilisema ni kwamba, anapoiangalia Azam anaifananisha na APR ya zamani iliyokuwa na nyota kama Mbuyu Twite, marehemu Patrick Mafisango, Kabange Twite, Haruna Niyonzima na Leonel Saint Preux.
Mnyarwanda huyo, anayecheza kwa ufasaha kiungo mkabaji na mara chache kiungo mshambuliaji, japo baada ya kutua Azam kocha Muingereza Stewart Hall amemwongezea jukumu la kucheza kama beki wa kati, anasema kwa ushindani aliouona Azam, anaamini itatisha Afrika kwa soka lake.
Mchezaji huyo mwenye umbo refu ni mume wa Gissa Fausta, mtangazaji wa kituo cha runinga cha Lemigo cha Rwanda akiwa ni baba wa mtoto mmoja wa kiume, Mugiraneza mwenye miezi saba, alifunguka mengi katika mahojiano na gazeti hili.
Kwa nini Azam?
Migi anasena alitua Azam na siyo klabu nyingine kutokana na kuvutiwa na misingi imara iliyopo katika klabu hiyo kwani alikuwa akiifuatilia kwa muda.
“Nimeamua kuja Azam kutokana na namna nilivyokuwa naisikia, ina misingi mizuri pia inawajali wachezaji, lakini mbali na hivyo, ni kutafuta changamoto baada ya kucheza ligi ya nyumbani kwa muda mrefu,” anasema.
“Kitu kingine kilichonishawishi ni maendeleo. Unajua nilikuwa nacheza na Niyonzima (Haruna) APR yeye akiwa pacha wangu, mimi nacheza kiungo mkabaji na yeye kiungo mshambuliaji na hata timu ya taifa ni vivyo hivyo, lakini kwa sasa mwenzangu amefanikiwa kwa kila kitu.
“Naamini nitakapocheza hapa kwa malengo, kiwango changu nitakipandisha na inaweza kuwa njia ya kutoka kwenda kucheza mbali zaidi katika nchi zilizofanikiwa kisoka.”
Post a Comment