Yanga imenoga sasa... Soma habari kamili

YANGA imefanikiwa kutumia ukongwe wake kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Friends Rangers ya Manzese, lakini katika mastaa waliosajiliwa waliokuwa wakiangaliwa, Malimi Busungu na kiungo Lansana Kamara, walionyesha kuwa kweli wanastahili kuvaa jezi ya timu hiyo.
Wachezaji hao walifanya mambo makubwa katika pambano hilo la kirafiki lililochezwa kwenye Uwanja wa Karume, jijini Dar es Salaam asubuhi ya jana Jumatano na kuhudhuriwa na mashabiki lukuki waliotaka kuona vijana wa Hans Pluijm wanafanya nini kwa Friends iliyoundwa na ‘mafaza’ wengi.
Katika mchezo huo ambao kocha wa Yanga, Pluijm aligoma usiitwe pambano na badala yake utambuliwe kama mazoezi, mabingwa hao walifanikiwa kupata bao lake la kwanza kupitia mshambuliaji Mliberia, Kpah Sherman katika dakika ya tisa akimalizia krosi safi ya Busungu.
Busungu alitoa pande hilo baada ya kugongeana vema na beki Juma Abdul na Sherman hakufanya ajizi kuweka ngoma kimiani, ingawa Friends ililisawazisha dakika ya 23 kupitia kiungo wao Mussa Juma kwa mkwaju wa adhabu ndogo iliyomuacha kipa Benedictor Tinocco akishangaa.
Kuingia kwa bao hilo kuliwaamsha Yanga na kufanikiwa kufanya mashambulizi makali na kufanikiwa kupata bao la pili dakika mbili kabla ya mapumziko kupitia Busungu akimalizia pasi ya Sherman matokeo ambayo yalibaki hadi wakati wa mapumziko.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko na Friends ikafanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia Cosmas Lewis ‘Balotelli’ katika dakika 81, lakini Busungu aliifichia aibu Yanga kwa kufunga bao la tatu akiunganisha kona safi iliyochongwa na Simon Msuva.
Kifupi Yanga ilionekana kuwa tishio safu ya mbele lakini ikiangushwa na ugeni wa Tinocco na kujichanganya kwa safu ya ulinzi ya timu hiyo.
KAMARA
AFANYA YAKE
Achana na ufundi wa kiasi uliofanywa na wachezaji wengine wapya waliosajiliwa na Yanga kama kinda Geofrey Mwashiuya na Deus Kaseke, kiungo Lansana Kamara naye alifanikiwa kuonyesha ufundi wake katika sehemu ya kiungo akipiga jumla ya pasi 43 ndani ya dakika 63 tu.
Katika pasi hizo, kiungo huyo alipiga 32 zilizofika bila ya kupotea wakati Salum Telela waliocheza pamoja kama viungo, alipiga 23 na kupoteza moja katika kipindi chote cha kwanza.
Kipindi cha pili ambapo Kamara alicheza kwa dakika 18 tu, alipiga pasi 11 na kupoteza mbili wakati Telela akipiga nane zilizofika na kupoteza moja.

No comments