Cech ndani ya Arsenal.. Soma habari kamili

KAMA ni kumla ng’ombe basi amebaki mkia. Na sasa umebaki muda mchache kabla ya golikipa wa Chelsea, Petr Cech kutua katika lango la Arsenal, hii ni kwa mujibu wa vyombo vingi vya habari Uingereza.
Cech, 33, amekubaliana maslahi binafsi na Arsenal ikiwamo suala la mshahara, lakini mpaka sasa kikwazo kidogo kilichopo ni mazungumzo baina ya Arsenal na Chelsea ambayo yataendelea wiki hii.
Mpaka sasa kiasi cha pesa za uhamisho huo hakijajulikana lakini uhamisho huo unatazamiwa kuwa wa pesa kamili, tofauti na awali ambapo kocha wa Chelsea, Jose Mourinho alikuwa anataka mchezaji mmoja wa Kiingereza kutoka Arsenal lakini wababe hao wa Emirates wamegoma.
Inadaiwa kuwa Cech amemshukuru mmiliki wa Chelsea tajiri, Roman Abramovich kwa kumruhusu kuhamia timu yoyote anayotaka baada ya kuitumia Chelsea kwa misimu 11 ya uaminifu mkubwa na kugeuka kuwa kipenzi cha mashabiki hao.
Hata hivyo, Cech ameamua kujiunga na Arsenal kwa ajili ya kuendelea kubaki katika jiji la London ambapo familia yake imetulia katika jiji hilo na watoto wake wanasoma katika shule za jiji hilo.
Cech amebakiza mkataba wa mwaka mmoja Chelsea, lakini amelazimika kutafuta timu nyingine baada ya kupoteza nafasi yake ya kudumu kwa kipa chipukizi wa Ubelgiji, Thibaut Courtois aliyerudi klabuni hapo baada ya kukipiga Atletico Madrid kwa mkopo wa miaka mitatu.
Kocha wa Chelsea, Mourinho angependa zaidi Cech aende PSG ya Ufaransa kwa ajili ya kutoiimarisha Arsenal ambayo inaonekana kuwa mpinzani wake wa karibu msimu ujao baada ya kuanza kuimarika misimu miwili iliyopita.
Mlinzi wa zamani wa Arsenal, Lauren Etame Mayer ambaye kwa sasa anaishi nchini Hispania alidokeza katika mtandao wake wa mawasiliano wa Twitter kuwa kipa huyo alikuwa anakwenda zake Arsenal.
“Kila la Kheri Cech. Kwa muda mrefu kumekuwa hakuna uimara katika nafasi hiyo na mchezaji mwingine imara anahamia kwa ajili ya kuwapa ubingwa wa England,” Aliandika Mayer.
Endapo kocha wa Arsenal, Arsene Wenger atafanikiwa kumnasa kipa huyo aliyeipa Chelsea ubingwa wa Ulaya mwaka 2012 huku pia akiwa na mataji matatu ya Ligi Kuu ya England itakuwa ni kutimiza ndoto zake.
Msimu wa 2001-02 kabla Cech hajajiunga na klabu ya Rennes akitokea klabu ya Sparta Prague ya kwao Czech, Wenger alijaribu kumnunua kipa huyo ambaye wakati huo alikuwa ana umri wa miaka 20 kwa ajili ya kuwa msaidizi wa kipa mkongwe, David Seaman, lakini Cech alishindwa kuhamia England kutokana na tatizo la vibali vya kazi

No comments